Makala Na Fatma M. Suleiman, Unguja
“Sijatokea kwenye familia yenye uzoefu wa kisiasa, nimepata hamasa kuionyesha jamii mwanamke anaweza kuwa kiongozi na kutatua changamoto za jamii Mwanamke ni mlezi, mbunifu na mwenye fikra pevu, kwa hiyo hakuna sababu ya kunizuia kuingia kwenye uongozi wa kisiasa.”
Kauli hii inaakisi Taarifa ya Baraza la Taifa la Wanawake, Tanzania, 2023 inayoeleza kwamba “Kuhakikisha usawa wa kijinsia katika uongozi si chaguo, bali ni wajibu wa kijamii.”
Rahima Said Abdallah ni mfano wa mwanamke jasiri aliyevunja vikwazo vya kijamii na kugombea nafasi ya uwakilishi kupitia Chama cha Ukombozi wa umma (CHAUMMA) Jimbo la Mwanakwerekwe katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Rahima ana miaka 26 amethibitisha kuwa uongozi haujali jinsia, bali ni uwezo, bidii na dhamira ya kweli ya kuwatumikia watu. Kupitia safari yake, amekuwa kielelezo cha matumaini mapya kwa wanawake na vijana wanaotamani kushiriki katika uongozi wa kisiasa nchini.
Rahima alizaliwa mwaka 1998 na kuanza masomo yake skuli ya Msingi Bububu hadi sekondari katika Skuli ya Tumekuja. Alijiunga na Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka na kuhitimu ngazi ya Cheti na Stashahada. Alitunukiwa Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Fedha katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Skuli ya biashara, Chwaka mwaka 2024
Akiwa ni mawanandoa mwenye mtoto mmoja, Rahima anasimamia majukumu yake ya kifamilia na kisiasa kwa ustadi mkubwa.
Safari ya kisiasa ilianza mwaka 2021 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo aligombea nafasi ya Muweka Hazina wa Baraza la Vijana Taifa, ambapo aliibuka mshindi kutokana na uadilifu na uaminifu wake.
CHADEMA ilimjengea uzoefu mkubwa wa utendaji wa chama na ushiriki wa vijana ambapo mwaka 2022, alipata Tuzo ya Mtendaji Bora wa Mwaka kutokana na mchango wake mkubwa katika uimarishaji wa shughuli za chama hicho.
Alihamia CHAUMMA mwaka 2025 akiwa ni Mkurugenzi wa Fedha Mipango na Uchumi afisi za Makao Makuu wapii
Rahima anaamini kuwa jamii inahitaji kiongozi muadilifu, mchapakazi, mwenye upendo na atakayesimama kuisemea jamii juu ya changamoto zinazowakabili.
“Mimi ni kijana, natamani kutimiza hayo na naamini uwezo ninao.” Alisema Rahima kwa hisia.
Kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa, Rahima alifanya kazi katika Zan Bottlers na Zan Air kama Mshika Fedha. Uzoefu huo ulimjenga katika nidhamu ya kazi, uwajibikaji, na kujiamini mambo ambayo yamekuwa nguzo muhimu katika uongozi wake wa kisiasa.
Kupitia juhudi zake, Rahima aliweza kumsaidia rafiki yake ambaye alikuwa na hamu ya kushiriki katika siasa lakini alikumbana na changamoto kutoka kwa familia yake. Kupitia mazungumzo, ushauri na ujasiri aliouonyesha alimtia moyo kutokata tamaa na kuendelea na malengo yake ya kisiasa.
Amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila aliye na dhamira njema ya kutimiza lengo lake anamsaidia kwa hali na mali, ikiwemo kusaidia usafiri kwa wenzake.
Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na maendeleo ili kufikia 50/50, hii ndio ndoto ya Rahima anayopigania katika harakati zake.
Changamoto ni sehemu ya maisha ambapo vikwazo vya rasilimali fedha, kukosa ushirikiano, kubezwa na kudharauliwa kwa jinsia na umri wake mdogo vilimkumba Rahima katika safari yake ya siasa.
Ni Dhahiri, kumpiga chura teke ni kumuongezea mwendo, mafunzo ya mbinu za uongozi, ushawishi na uchechemuzi ya TAMWA yaliongeza mori na hamasa ya kuendelea kujiamini katika safari yake.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 Ibara 23-25 inabainisha wazi dhana ya mwanamke katika nafasi za uongozi. Hili ndilo lililomsukuma zaid Rahima kupata mafanikio sambamba na kutekeleza kwa vitendo ule msemo wa jungu kuu halikosi ukoko. Kwani ushauri wa viongozi wanawake waliomtangulia akiwemo Katherin Ruga na kujenga mtandao ilikuwa ndio siri ya mafanikio yake.
Bi Arafa Said ni mama mzazi wa Rahima anaeleza kuwa
“anachokifanya Rahima ni jambo la kuigwa katika jamii, hasa kwa wanawake. Kupitia yeye, tutaweza kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika majimbo yetu.”
Msimamo huu wa familia umekuwa msaada mkubwa kwa Rahima katika kufanya maamuzi ya kisiasa bila woga.
Suleiman Asaa Kheri, mtendaji wa Makao Makuu ya CHAUMMA, anaeleza:
“Rahima ana ushawishi mkubwa kwa vijana amewahamasisha wengi kujiunga na siasa jambo lililoleta mageuzi makubwa ndani ya chama.”
“Rahima ni mtu wa kujitolea na anayepambana bila hofu. Ni kielelezo kwangu kama mwanamke.”
Kwa upande wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, wengi wameonyesha imani kubwa kwake, “Tunayo matarajio mengi kwake, na mengine tayari yameanza kufanikishwa. Uthubutu wake na kujiamini kwake ni ishara ya maendeleo.” Alisema Mwanakhamis Maulid
Rahima ana ndoto ya kuona kizazi kipya cha wanawake kinashika hatamu za uongozi na kufanya maamuzi muhimu kwa maendeleo ya taifa. Anaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika uongozi ni nguzo ya demokrasia na maendeleo endelevu.
Kwa hakika, Rahima Said Abdallah anabaki kuwa mwanamke jasiri, kiongozi shupavu, na mfano wa kuigwa katika siasa za kizazi kipya cha Tanzania.
MWISHO

Comments
Post a Comment