NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA
Msemo unaosema hata “Mbuyu Ulianza Kama Mchicha” umesadifu kwa Makamo Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu Taifa na Mjumbe wa halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo Mkunga Hamad Sadala Mkaazi wa Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba ambaye pia ni Mama wa Watoto tisa.
Bi. Mkunga alianza kujitumbukiza kwenye dimbwi la siasa mwaka 1992 wakati ambao mfumo wa vyama vingi Nchini Tanzania ndio kwanza unaanza kwa kujiunga na Chama Civil United Front (CUF) na safari ya Bi. Mkunga kisiasa ikaanzia hapo akiwa na umri mdogo huku akiwa mtumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kada ya ualimu katika Skuli ya msingi iliopo Vitongoji na kukumbana na dhoruba kali ya kimbunga cha kujiunga na Siasa ya upinzani ambayo ilikuwa ni mwiko kwa watumishi wa umma ambayo ilitamalaki zaidi Kisiwani Pemba kwa kipindi hicho.
Lakini moyo wa uzalendo na ujasiri ulimsukuma kuruka vihunzi hivyo na sasa kuwa mwanamke wa kupigiwa mfano Visiwani Zanzibar.
![]() |
VIHUNZI ALIVYOKUMBANA NAVYO
Suala la mfumo dume katika vyama vya Siasa ni moja miongoni mwa vihunzi ambavyo Bi. Mkunga amepitia anatia nia ya kugombea nafasi ya uongozi katika chama chake cha CUF ambapo mwanamke anapotia nia ya kugombea nafasi ya Udiwani, Uwakilishi au Ubunge huonekana hawana uwezo wa kugombea nafasi hizo na badala yake hupokea ushauri kwa wanachama wenzao wanaume kuwashauri kugombea nafasi ya Viti Maalum badala ya nafasi za Serikali.
MAONI YA VIONGOZI WA ACT WAZALENDO
Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa Chaka Chake na Mjumbe wa Halmashauri Mkuu Saleh Nassor Juma, amesema Bi. Mkunga ni miongoni mwa Wanawake wa na tegemezi ndani ya Chama cha ACT Wazalendo kutokana na ujasiri na msimamo ambao unawafanya wanawake wengine wahamasike kujiunga na chama hicho bila ya kujali maslahi binafsi na changamoto wanazopitia
Amesema “Kwa hakika Bi. Mkunga ni hakiba ya kudumu ndani ya ACT Wazalendo kutokana na uthabiti na uzalendo wake tumetoka mbali sana hata kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo na hajawahi kuyumba wala kuetetereka licha ya kupitia mazito tangu akiwa chama cha wananchi CUF”
MAONI YA WANACHAMA WENZAKE
Faki Mohammed Sheha ni Mkaazi wa Vitongoji na mwanacha wa ACT Wazalendo amesema “kwakweli naweza kusema kwetu ni faraja kubwa kuwa mwanachama na kiongozi mwenye msimamo, ujasiri na uthubutu kama Bi. Mkunga kwakweli ni kiongozi wa mfano kwasababu kuna mambo muda mwengine tunahisi kama hayawezekani ila yeye anasema inawezekana”
VIONGOZI WA ASASI ZA KIRAIA
Mkurugenzi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi (SWIL) kutoka Jumuiya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) Hafidh Abdi Said, amesema “Bi. Mkunga ni miongoni mwa matunda tuliyoyazalisha kupitia mradi wa kuwawezesha Wanawake kushiriki katika mambo ya Sias ana Uongozi yani mradi wa SWIL ulioanza mwaka 2020, yeye alikuwa wanawake wa kwanza kufikiwa na mradi huo kwa kupatiwa mafunzo mbali mbali yaliyomjenga na kumuimarisha zaidi kisiasa na kiutendaji hadi kuwa mwanamke wa mfano Pemba kwenye mambo ya siasa na Uongozi”
MAISHA YAKE YA KISIASA NA FAMILIA
Watu wengi hudhani mwanamke anapoingia kwenye siasa ni mwanzo wa kuitelekeza familia yake kutoka harakati za kisiasa jambo ambali sio sahihi, Bi. Mkunga anasema harakati za kisiasa hazijawahi kumteteresha kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu ya familia yake kwani anapotoka kwenye kwenye ujenzi wa chama kila huwa katika mpangilo wake.
MUME WAKE ANAMZUNGUMZIAJE?
Salum Mbarouk Shaame ni mume wa Bi. Mkunga ambaye nae pia ni mwanachama wa ACT Wazalendo, amesema licha ya kuwepo kwa dhana kuwa wanawake wanapojiunga na vyama vya siasa na kugombea nafasi za uongozi hubadilika kitabia ikiwemo kuwadharau na kuwaendea kinyume waume zao lakini kwake hajawahi kuona mabadiliko hayo na kusisitiza kuwa ataendelea kumuunga mkono katika harakati zake kisiasa
Amesema “Binafsi tangu nifunge nae ndoa sijawahi kuona mabadiliko yoyote mabaya alionifanyia kutokana na shughuli zake hizi za kisiasa ananiheshimu kama mume wake na tuhaheshimiana na nitaendelea kuwa pamoja nae kwenye harakati zake za kisiasa mpaka atakapoamua mwenye kustaafu”
WATOTO WAKE WANAMZUNGUMZIAJE?
Ramadhan Salum Mbarouk ni mtoto wa pili wa Bi. Mkunga amesema amejifunza mengi kutoka kwa Nguli huyo wa Siasa za upinzani (Mama yake) ikiwemo kujiamini, uthubutu, uzalendo na ujasiri wa kusimamia maslahi ya umma kwa kukataa maslahi binafsi licha ya kukumbana na milima na mabonde ambayo yalimkosesha usingizi baadhi ya nyakati.
MAONI YA MAJIRANI ZAKE
Halima Said Abrahman ni jirani wakuombana chumvi na sukari na Bi. Mkunga amemuambia mwandishi wa Habari hizi kuwa licha ya umaarufu alionao kwenye medani za siasa lakini muamala wake mzuri na majirani zake na jamii ni miongoni mwa mambo yanayomfanya akubalike zaidi kisiasa na kijamii
“licha ya umaarufu wake cheo chake na elimu yake lakini bado anaishi na watu vizuri sana kila mtu kwake ni ndugu rafiki na mwana hana ubaguzi au kujisikia mambo hanawafanya watu wamkubali sana na mimi nakuahidi endapo atagombea nafasi yoyote hata kwenye hicho chake cha ACT basi hata CCM watamtilia kura” Fatma Hamad Ali- jirani




Comments
Post a Comment