NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA
Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania umekutana na wadau mbali mbali Kisiwani Pemba wakiwemo Viongozi wa Jumuiya zisizo za Kiserikali (NGOs), Wahamasishaji wajamii(CBs) Waandishi wa Habari pamoja na Wagombea Wanawake kutoka vyama vya Siasa kujadili Mafanikio yanayotokana na Mradi wa Uhamasishaji Wanawake kushiriki katika nafasi za Uongozi, Strength Women In Leadership (SWIL).
Akizungumza na wadau hao huko katika Ofisi za TAMWA Mkanjuni Pemba Balozi Norway Tanzania Tonnis Tinnes, amesema ripoti zinaonesha mradi huo umewawesha wanawake zaidi ya elfu mbili kupata elimu na hamasa ya kushiriki katika vyama vya siasa na uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Aidha Balozi Tonnis huyo amesema Ubalozi Norway Tanzania utaendelea kushirikiana na wadau hao katika kukuza na kuongeza ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi.
Mshauri Mkuu wa Masuala ya Jinsia Anette Otilie kutoka Norway, amesema Ushiriki wa Wanawake katika Siasa, Uongozi na Demokrasia kusaidia katika kwa kiasi kikubwa kukuza usawa wa kijinsia kuanzia ngazi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) upande wa Zanzibar Mzuri Issa, amesema mradi wa SWIL umeleta mwanga wa mabadiliko chanya Visiwani Zanzibar katika dhana ya Wanawake na Uongozi kutokana hali iliyosaidia kuongeza idadi ya wanawake kuongezeka maradufu katika Shughuli za Kisiasa na Maendeleo.
Nae Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakari Mussa, amawashukuru waendashaji wa mradi huo kutokana na mafunzo mbali mbali waliowapatia juu ya Uwezeshaji wa Wanawake katika Sias ana Uongozi sambamba na kuwapa tunzo waandishi waliofanya vizuri katika mradi huo.
“Na sasa hivi sisi watu wa Habari niseme tumefaidika kwasababu waandishi wengi kisiwani Pemba wana uwezo nzuri wa kuandika Habari za wanawake zenye kuleta tija kwao na kwa taifa kwa ujumla” Mwenyekiti PPC, Bakari Mussa
Nao Wahamasishaji Jamii (Citizen Brigade) na Wanaume wa Mabadiliko (Male Change Agent) wameupongeza Ubalozi wa Norway Tanzania na Tamwa, Zanzibar kwa jitihada zao za kuelimisha jamii juu haki za Wanawake ikiwemo kushiriki katika Demokrasia na Uongozi elimu ambayo imechangia idadi ya wanawake waliogombania nafasi mbali mbali za uongozi kuelekea Uchaguzi wa 2025 kuongezeka maradufu.
“Niwapongeze kwa mradi huu ule mwaka 2019 haikuwa rahisi katika Visiwa hivi vya Unguja na Pemba kuwaambia mwanamke kushiriki katika uongozi sio kazi rahisi, lakini tunaona leo TAMWA wametoa Kitabu hichi kinachoelezea wanawake kushiriki katika na Uongozi na wakatoa na muongozo wa Viongozi wa dini kuhusu uchaguzi na laiti fomu ya Urais isingekuwa laki tano wanawake wote wangegombea” Omar Mjaka Ali, mwanamme wa mabadiliko kutoka Kilindi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) Tatu Abdalla Msellem, amesema Taasisi ya TUJIPE imenufaika kwa kikubwa kupitia mradi wa SWIL kwa kutoa elimu ya Uongozi kwa Viongozi na watendaji wa Taasisi hiyo pamoja na kuwaomba wadau hao kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kuendeleza mradi huo.
“Binafsi niseme TUJIPE tumefarajika sana katika awamu zote mbili za mradi huu wa SWIL awamu ya kwanza tulishirikishwa kikamilifu kama NGOs tukawa tunashiriki katika kazi mbali mbali ikiwemo kutoa elimu katika jamii ambapo kuna wadau wengi tuliwafikia wengi wao wakiwa ni wanawake” alifafanua
Wakitoa neno la shukurani kwa waendeshaji wa mradi wa SWIL wagombea Wanawake kutoka vyama mbali mbali vya Siasa, wamesema elimu na hamasa walizopata kutoka kwa wadau wa mradi huo ndio nguvu pekee iliyowawezesha kujiamini na kuwa na uthubutu wa kugombania nafasi mbali mbali ikiwemo Urais, Ubunge, Uwakishi na Udiwani.
“Mimi ni Mgombea wa chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMA nimeshikwa mkono na TAMWA, PEGAO NA ZAFELA kusema kweli tumepata mafunzo mazuri nilikuwa siwezi kusimama nikasema chochote lakini sasa naweza kusema popote nikasema chochote lakini sasa naweza, kwa maana hiyo elimu na hamasa iliyotolewa na jumuiya hizi ni kubwa mno” Mariam Saleh Juma kutoka Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA)
Mradi wa Uhamasishaji Wanawake kushiriki katika nafasi za Uongozi, Strength Women In Leadership (SWIL) Zanzibar, ulianzishwa mwaka 2020 unatekelezwa na TAMWA, ZANZIBAR, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZAFELA) Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsi na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania.






Comments
Post a Comment