Skip to main content

WAANDISHI WA HABARI PEMBA WABEBESHWA ZIGO LA “AMANI” KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA 2025.

NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA

Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba wametakiwa kuzingatia weledi, maadili na taaluma ya Habari katika kuandika na kuripoti taarifa zinazochochea amani na utulivu nchini.

Akizungumza na Waandishi hao katika Ukumbu wa Baraza la Mji Chake Chake Afisa mdhamini Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau katika Kongamano la Kuimarisha Amani kati ya Jeshi Polisi na Vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, amesema waandishi walioshiriki katika Kongamano hilo wanapaswa kuzingatia maelekelezo waliyopatiwa katika kipindi cha Uchaguzi.

Aidha Afisa huyo ameliomba Jeshi la Polisi kuwashughulikia Waandishi watakaokiuka maelekezo yaliyotolewa kwenye Kongamono ili iwe mfano kwa waandishi wengine.

“Kwa habati mzuri hapa munazungumza Kiswahili kimoja lakini mukikutana fild (eneo la kazi) katika wale watu ambao mumewapa maelekezo halafu mukaja kugundua wale watu wambao tumekaa tumedicuss nao haya mambo umuhimu wa amani kuelekea katika kipindi cha Uchaguzi halafu mule miongoni mwao mwandishi wa Habari mukamkuta kaingia katika shida sasa niwaombeni sana mtu kama huyo wala musimuache mumshughulikie vizuri sana, yes narejea tena naomba hii moni note vizuri sana sasa niwaombe sana Jeshi la Polisi kwenye hili jambo musiwe na muhali wala musimuone mtu huruma kwasababu hakuna mbadala kwenye Amani” alisema

Akifungua Kongamano hilo Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kombo Khamis Kombo ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari ni nguzo muhimu katika kujenga amani na mshikamano kuelekea uchaguzi wa 2025”

“Nadhani sote ni mashahidi yaliyotokea na yanayoendelea katika taifa mbali mbali duniani baada ya amani kutoweka, hivyo basi kwa umoja wetu na taaluma zetu tunapaswa kuwa na mashirikiano ya karibu katika kuhakikisha tunaitunza na kuilinda amani na mashirikiano tuliyonayo katika taifa letu katiki kipindi chote cha uchaguzi na baada” Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kombo Khamis Kombo

Akiwasilisha mada ya Miiko na Maadili ya Vyombo vya Habari kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja, amewataka waandishi hao kutumia taaluma yao kwa weledi kuripoti matukio yanayojiri kipindi cha uchaguzi ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.

“Niwasihi tu licha ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kutupa fursa ya kupokea na kutoa taarifa bila ya kuathiri Usalama wa Taifa nyinyi kama waandishi munapaswa kutumia taaluma na weledi mulionao katika kuripoti matukio ambayo hayatochochea machafuko na taharuki kwa taifa” Mkuu wa Wilaya Micheweni Khatib Juma Mjaja

Kwa upande Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba Ali Mbarouk, amewasihi wanahabari hao kuzichuja taarifa zao kabla ya kuzichapisha na kuzirusha kwenye vyombo sambamba na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa za uzushi na uongo.

“Hata kama ni taarifa ulionayo nayo ni kweli lakini kama mwandishi wa Habari unapaswa kuzichuja taarifa zako kabla kuzirusha pamoja kujiuliza je, Habari hii nikitoa italeta athari gani kwa Taifa? Tutamubue kuwa hakuna Habari kubwa kama usalama wako na taifa upo hatarini” Ali Mbarouk Katika PPC

Wakichangia mada na hoja mbali mbali juu ya Kongamano hilo baadhi ya wanahabri hao wamesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya Makamanda wa Jeshi la Polisi kutokutoa ushirikiano kwa waandishi wa Habari hali inayochangia kuwarudisha nyuma waandishi hao kufanya kazi kwa ukaribu na Jeshi hilo.

“Kwakweli waandishi wa Habari Pemba tunakabiliwa changamoto nyingi sana miongoni mwa changamoto hizo ni kwa upande wa Jeshi la Polisi baadhi ya Makamanda wa Mikoa hawana mashirikiano na sisi waandishi unatafuta balance (usawa) kwa Jeshi la Polisi kuhusu tukio fulani mwezi mzima unaambiwa mara kamanda hayupo mara yupo busy mpaka unakata tamaa unaamua kuifanya hiyo Habari pasi na kauli ya Kamanda hiyo hali inaturudisha nyuma sana kwakweli” Fatma Faki Salim, Mwandishi kutoka Blog ya Pemba ya Leo

Suala la usalama kwa waandishi wa Habari katika kipindi cha kupiga kura ni miongoni mwa hoja iliyoibuka ambapo waandishi walisema kumekuwepo na matukio kadhaa ya waandishi wa Habari kutishiwa amani na maafisa wa Jeshi la Polisi wakati wanatekeleza majukumu hali inayosababisha kushindwa kutuekeleza majukumu yao ipaswavyo.

“Kwa miongo tofauti kumekuwepo na matukio ya waandishi wa Habari kutishiwa amani na watu ambao tunashindwa kufahamu kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi ama laa maana hata mavazi yao sio ya Kipolisi, baadhi yao wameficha sura (mazombi) lakini wanatumia magari ya poilisi na vikosi sasa kwakweli hali hiyo inatupa wakati mgumu sana waandishi wa Habari kipindi cha Uchaguzi” Is-haka Mohammed Rubea, mwandishI Zenj Fm Radio

Akitoa ufafanuzi juu ya hoja hizo Mkuu wa Polisi Jamii Kamisheni ya Polisi Zanzibar Kamishna Mwandamizi wa Polisi SACP Jonas Mahanga, ali0wataka waandishi hao kutoa taarifa kwa viongozi wa Jeshi la Polisi pindi wanaoona viashiria vyovyote vya kuvunjiwa usalama wao pamoja kuizuliwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Kongamano hilo lenye lengo la Kuimarisha Amani Kupitia Hoja Na Mijadala Ya Maelewano Baina Jeshi La Polisi Na Vyombo Vya Habari Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025” limebeba Kauli Mbiu inayosema

“AMANI, UTULIVU, NA USALAMA KABLA YA WAKATI, NA BAADA YA UCHAGUZI 2025 NI JUKUMU LETU SOTE”



Comments