NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA
Visa vya Watoto kuzaliwa kutelekezwa na kutupwa vinaendelea kuchukua nafasi Kisiwani Pemba, hii ni baada ya mtoto mchanga wakike anaekadiriwa kuwa na wiki moja kukutwa ametelekezwa mbepezoni mwa Msikiti wa Mkanjuni Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Akisimulia kuhusu tukio hilo Sheha Mkoroshoni Zuwena Suleiman Salahi, alisema siku ya Ijumaa Agosti 29.08.2025 saa 1:30 usiku alipata taarifa kutoka kwa mjumbe wake za kuonekana kwa mtoto huyo akiwa ametelekezwa na mtu asiefahamika.
Aidha Sheha huyo ametoa wito kwa wanawake kuacha tabia za kuwatelekeza na kuwatupa Watoto kwa kuhisi aibu ya kuzaa nje ya ndoa au sababu nyenginezo kwani kufanya hivyo ni kinyume na Sheria za Serikali na Dini.
“Jana siku ya Ijumaa saa 1:30 usiku nilipata taarifa kutoka kwa mjumbe wangu wa sheha kuwa kuna mtoto ametupwa msikiti mkanjuni ndio nikatoka nikaenda nilipofika mtoto alikuwa ameshaondoshwa pale msikitini yupo kwa mjumbe wangu wa sheha nikenda kumuona kisha nikampigia simu Mkuu wa Wilaya nikawapata taarifa Jeshi la Polisi nikamchukua nikampeleka hospitali akafanyiwa vipimo baada ya kufanyiwa vipimo nikarudi nae nyumbani” alisema
Akitoa ufafanuzi kuhusu jukumu la Ustawi wa Jamii kwa Watoto wanaotelekezwa na kutupwa, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mkoani Zuwena Mohammed Mussa, alisema jukumu la Ustawi wa jamii ni kuwatunza na kuwalea Watoto hao kupitia walezi wa malezi (Foster Parent) ambao wanapatikana kila Shehia.
“Kama ikitokea mtoto katelekezwa au katupwa sisi tuna walezi wa malezi (Foster Parent) hawa walezi wa malezi ambao tunawaweka kila Shehia jukumu lao hao ni kuwatunza Watoto hao ili kuwaepesha na madhara ambayo yanaweza kumpata kwa kipindi hicho na hapo atakuwa chini ya uangalizi wa Afisa ustawi wa Wilaya husika na atakaa hapo kwa kipindi tukiwa tunafuatilia je, kuna uwezekano wa kuipata familia yake kwasababu sisi Ustawi tunasema malezi bora ni kwa wazazi, sasa ikiwa haitokea familia au mtu wa karibu sasa hapo ndipo Mkurugenzi Ustawi ataamua wapi ampeleke na kumpeleka ni Unguja kwenye vituo vya kulelea Watoto kwasababu Pemba hatuna vituo hivyo” alifafanua Afisa huyo
Ikumbukwe kuwa July 30.2025 Amina Rashid Abass miaka 22, mkaazi wa Michakweni Shehia ya Kiwani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujifungua na kumtupa mtoto kwenye shimo la choo na kufariki Dunia.

Comments
Post a Comment