NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA
"AMINA" KINARA
WA UOGELEAJI BONANZA LA UTALII PEMBA
Na, Hassan Msellem, Pemba
Ni msichana wa miaka 15,
Mkaazi wa Tumbe Mashariki anayesoma kidato cha Pili aliwashangaza wengi
walioshiriki mashindo ya mchezo wa kuogelea yaliyofanyika huko Vuma Wimbi
katika Pwani ya Msuka Kaskazini mwa Kisiwa Cha Pemba kwa kipawa chake cha kupiga
mbizi na kuwashinda wapiga mbizi wenzake 14 na hatimae kuibuka mshindi wa pili.
Msichana huyo mwenye umri
mdogo zaidi kuliko waogeleaji wote walioshiriki mchezo huo aliwaacha vinywa
wazi watu wote waliokuwa wakishuhudia mtanange huo wapasua maji pasi na msaaada
wowote wa waongoza mashindano hayo yaliyojumuisha urefu wa mita 20
Baada ya ushindi huo
mwandishi wa Makala hii alipata nafasi ya kuzungumza na msichana huyo
ilikufahamu siri ya kuibuka mshindi wa pili na kusema kufanya mazoezi kwa bidii
ndio siri pekee iliyofanya awe na uwezo wa kupasua mawimbi zaidi kuliko wenzake
ambao walionekana mapafu yao kukomaa zaidi na kwamba ndoto yake ni kuwa mpiga mbizi
maarufu kisiwani Pemba na Zanzibar kwa ujumla
“kwakweli siri ya kuibuka
mshindi ni kufanya mazoezi kwa bidii mimi na wenzangu hua tunafanya mazoezi
kila siku jioni hasa siku za Jumamosi na Jumapili ambazo siendi Skuli” alisema
Amesema Kitita cha
Shilingi laki saba kimempa shauku na hamasa ya kuendelea kufanya mazoezi kwa
bidii zaidi na kujipanga na mashindano mengine mwakani na kila fursa ya
mashindano inapotokea
“kwakweli fedha hizi
zimenipa hamasa sana sasa ya kuamini kuwa mchezo wa kuogelea unalipa na sio
mimi hata wenzangu pia kwahivyo tunaahidi kuzidisha bidii ya kufanya mazoezi
ili kuendelea kufanya vizuri mwakani na kila inapotokea fursa ya mashindano”
alisema msichana Amina
Amefafanua kuwa hakuweza
kuamini kuwa ataweza kuibuka mshindi wa pili kwa kumshinda na mchezaji kutoka
kikosi cha JKU Zanzibar ambaye hawalingani na kimo chake wala umri wake, ambaye
aliibuka mshindi wa kwanza.
Kaije Seif Bakari ni mwalimu
wa kikosi cha timu ya kuogelea ya Tumbe Mashariki ambayo msichana Amina
anashiriki, amesema timu yao imekuwa ikifanya vizuri katika mashindo mengi na kuvutia
watu wengi kutokana na umahiri wao wakuogelea na kuwepo kwa muogeleaji mdogo huyo
mwenye kipaji cha ajabu
“kwakweli timu yetu ni
mzuri sana kwasababu mashindano mengi tunayoshiriki tunashinda na watu wengi
wanavutiwa na uwezo wetu wa kuogelea na kushiriki katika mashindano haya
tunajisikia Faraja sana na tunaahidi kufanya vizuri zaidi kwa mashindano
yajayo”
Bi. Kaije anasema wakati
wanaanzisha klabu hiyo yenye jumla ya wanawake kumi wanaoogelea walipitia
wakati mgumu kwani walikosa ushirikiano kutoka kwa jamii kwa kile wanachoamini
kuwa wanawake hawapaswi kushiriki mchezo wa kuogelea kama wanaume
‘’Tumeanzisha timu hii
lakini hatukuwa tunakubalika katika jamii tulionekana kama tumekosa kazi au
wahuni tu lakini hatukurudi nyuma na tukaendelea kujipa moyo na kufanya mazoezi
zaidi kwani tulikuwa na malengo yetu ikiwemo kujiokoa pindi inapotokea ajali ya
kuzama maana sisi ni wavuvi lakini pia tuliamini ipo siku tutajipatia kipato
kupitia kuogelea na leo tumeshuhudia tayari tumepata shilingi laki saba sio
kidogo” Bi. Kaije
Kwa upande wake Maratibu
wa Kamisheni ya Utalii Kisiwani Pemba Hamad Amini, amesema walipata taarifa ya
kuwepo kwa kikundi cha akina mama hao kupitia mwandishi Blog ya Pemba Post na
ripota wa Mawio Hassan Msellem ambaye aliwaibua akina mama hao ndipo nao
walipoonda kuna haja ya kuwatambua na kuwaunga mkono kwa kuwapa fursa ya
kushiriki katika mashindano hayo ya Bonanza la Utalii Pemba ili kuonesha uwezo
walionao na kutoa motisha kwa wanawake wengine Kisiwani Pemba
‘’Ni miaka mingi sana
tulikuwa tunafanya Bonanza hili lakini hatukuwahi kuwa na kikundi ya wanawake
wanaogelea Pemba lakini kuwepo kwa kikundi hicho kwakweli ni faraja kubwa,
taarifa za kuwepo kwa kikundi hichi nilizipata kutoka kwa mwandishi wa Habari
Hassan Msellem ambaye alikuja ofisini kwetu na akanipa taarifa za kuwepo kwa
akina mama hawa ndipo tukapanga kwenda kuwaona na kweli tulikutana nao na
tukawaahidi kushiriki katika mashindano ya kuogelea katika Bonanza la Utalii
Pemba linalofanyika Novemba kila mwaka” mratibu wa Kamisheni ya Utalii Pemba
Alisema licha ya kuwa ni
mara ya kwanza kutoa fursa kwa wanawake kuonesha uwezo wao wa kuogelea lakini wameonesha
uwezo nzuri katika mchezo huo na kuwavutia wengi na kuahidi kuendelea kutoa
fursa kwa wasichana na wanawake mashindano hayo kila mwaka ili kujipatia fursa
za maendeleo
Kuibuliwa kwa kikundi
hicho cha akina wanawake wanaoshiriki vyema mchezo wa kuogelea kumetokana na
uendeshwaji wa mradi wa usawa wa kijinsi kwenye michezo visiwani Zanzibar unaosimamiwa
na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) upande wa Zanzibar
kwa lengo la kuhakikisha wasichana na wanawake wapata haki sawa ya kushiriki
katika michezo
Khairat Haji Ali, kutoka
Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar amesema Tamwa
imekuwa ikikutana na makundi mbali mbali ya wananchi na watendaji wa Serikali
na taasisi za Kiraia katika kujenga uwelewa zaidi kwa jinsia ya kike
kushirikishwa katika michezo ili kuimarisha ustawi wao
“Kwa muda mrefu tumeona
wasichana na wanawake wanakosa fursa ya kushiriki na kushirikishwa katika
masuala ya michezo, hivyo basi tumeona sasa ni muda muafaka wa kukaa pamoja
jamii, Serikali na taasisi za kiraia ili kujenga uwelewa wa kuwashirikisha
wanawake kwenye michezo ili kuimarisha ustawi wanawake katika Nyanja mbali
mbali ikiwemo afya na maendeleo” alisema
MWISHO.

Comments
Post a Comment