TAMWA ZNZ, ZAFELA, CYD na GIZ waipongeza Timu ya WARRIOR QUEEN kushiriki mechi ya Klabu Bingwa Afrika, Ethiopia.
Watekelezaji
wa program ya Michezo kwa Maendeleo Zanzibar (S4D) wanawatakia kila la kheri
timu ya Warrior Queens ya Saateni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja katika
mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa upande wa ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati (CECAFA) yanayotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia kuanzia tarehe 17 mpaka
tarehe 31 Agosti mwaka huu 2024.
Timu
ya Warrior Queens itaiwakilisha Zanzibar katika mashindano hayo na inatarajiwa
kuondoka nchini kuelekea Ethiopia siku ya Alkhamis, tarehe 15 Agosti 2024. Tunaamini
kuwa wataiwakilisha Zanzibar kwa fahari kubwa na kurudi nyumbani wakiwa
washindi.
Pamoja
na kuwapongeza wadau wote waliofanikisha timu hii kukamilisha mahitaji ya
safari hiyo, TAMWA ZNZ inasisitiza umuhimu kwa wadau wote kuendeleza usawa wa
kijinsia kwa kuzisaidia timu za wanawake na kukuza vipaji vyao ili kujenga
jamii inayothamini na kuinua michango ya wanawake.
Bado
ipo haja kwa wadau wote wa michezo, ikiwemo serikali, taasisi binafsi, na wadau
wengine, kuongeza nguvu katika kuzisaidia timu za wanawake ili kuwawezesha
wachezaji wetu wa kike kushiriki na kushinda mashindano mbalimbali, ndani na
nje ya nchi.
Kufuzu
kwa klabu ya WARRIOR QUEENS kwenye mashindano hayo kunatokana na klabu hiyo
kuchukua ubingwa wa ligi kuu soka Zanzibar upande wa wanawake msimu wa 2023/2024
ambapo jumla ya timu 10 za wanawake zilishiriki.
Program
ya S4D inatekelezwa kwa mashirikiano na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar
(ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), kwa mashirikiano makubwa na
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ujerumani - (GIZ) - chini ya Wizara ya
Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ).
Kila
la kheri WARRIOR QUEENS!!!
Comments
Post a Comment