Makala Na, Hassan Msellem- Pemba
Kuogelea ni miongoni mwa michezo maarufu duniani na ni mchezo unaoshindaniwa kikanda, kitaifa na hata kidunia.
Lakini linapokuja suala kuogelea machoni mwa wengi tunawaona wanaume pekee ndio washiriki vinara wa mchezo huo, licha ya uchache wao wapo kwa Wanawake ambao wana uwezo na vipaji vya hali ya juu katika mchezo wa kuogelea.
Hamu na shauku ya Kaije ni kuwa kama Nguli wa mchezo wa kuogelea Dunia Bakulaben Patel mwanamke mwenye umri wa miaka 80 ni bingwa wa kuogolea kutoka Surat Magharibi mwa India, ambaye alianza kuogelea akiwa na umri wa miaka 58 na tangu wakati huo ameshinda karibu medali 500 katika mashindano ya kitaifa na kimataifa. Pamoja na hamu ya kuwafundisha wengine, anataka kuweka rekodi ya dunia.
Kwa
mujibu wa ripoti ya shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (fina) zaidi ya
nchi 80 hushiriki mashindano ya kuogelea huku mataifa kama vile finland,
australia, japan, urusi na marekani yakiongoza katika mashindano hayo
yanayojumuisha zaidi ya waogeleaji 200 huku wanawake wakiwa asilimia 30 tu hali
inayoashiria idadi ndogo ya ushiriki wa wanawake katika mashindano hayo.
Kila
mchezo hua na mitindo na mwembwembwe zake za kucheza na mchezo wa kuogelea nao
una mitindo mbali mbali kama vile freestyle, backostroke, breaststroke,
butterfly na side stroke.
Licha
ya gwiji wa kuogelea kwa sasa kaije said bakari wapo wanawake ambao waliwahi
kushika hatamu kupitia mchezo wa kuogelea kisiwani pemba akiwemo bi. Hija kombo
kutoka kojani, rukia omar kutoka kisiwa cha kokota, time haji kutoka kijiji cha
shamiani mwambe, mwanaidi kaasim kutoka kisiwa panza na maimuna juma kutoka
kisiwa cha makoongwe.
Kaije Said Bakari ni mama aliyebarikiwa watoto saba akiwa na umri wa miaka 32, anaishi Kijiji cha Tumbe Mbuyuni Shehia ya Tumbe Mashariki Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, ni nguli wa mchezo wa kuogelea sio kwa mji wa Tumbe tu bali hata Kisiwa cha Pemba kwa ujumla na mwalimu mchezo wa kuogelea kwa wanawake wenzake zaidi ya mia tatu Kisiwani Pemba.
Kipaji cha Kaije cha kuwa mashuhuri wa kupiga mbizi kiliibuka kupitia mradi wa The Panje ambao uliotoa fursa ya mafunzo ya
kuogelea kwa wanawake 20 wa Mji wa Tumbe, na Kajie kuibuka kinara kwenye mafunzo hayo na kupatiwa fursa ya mafunzo mengine ya kuogelea yaliyofahamika kwa jina la master training na hapo ndipo
nyota ya Kaije ya kupiga mbizi ikaanza kung’aa.
Zaidi ya wanawake na wasichana 335 kutoka maeneo mbali mbali Kisiwani Pemba walipatiwa mafunzo ya kuogelea kutoka kwa Bi. Kaije na kuwa na uwezo mzuri wa kuogelea na kushiriki mashindano na mabonanza na kupata zawadi zilizowafanya kuwapa ari, moyo na hamasa ya kupenda mchezo wa kuogelea.
“Nimefanikiwa kutoa mafunzo ya
kuogelea kwa wanawake na wasichana zaidi ya 300 maeneo mbali mbali kwa wanawake
na wanafunzi wa skuli ikiwemo hapa petu Tumbe wanawake 100 wanafunzi 60, Fundo
wanawake 30, Njau wanawake 20 na wanafunzi 120, Shumba Mjini 20, Tundauwa
wanawake 15, Makangale wanawake 10, Kojani walimu 4 na wanafunzi 16, Chwale
walimu 4 na wanafunzi 16” alisema
Mchezo wa kuogelea umemtoa Kaije
katika dimbwi la ufukara na umasikini wa kiwango cha juu na kumfanya aishi
Maisha ya kati na kati kwani umefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa ya tofali
badala ya kuishi kwenye hema na familia yake kama mkimbizi, kumpa mkate wake wa
kila siku pamoja na kusomesha Watoto wake.
“Mchezo wa kuogelea umenitoa mbali sana nilikuwa fukara sana nilikuwa naishi kwenye banda ambalo ni saw ana hema kama mkimbizi mimi na familia yangu lakini nashukuru kupitia mchezo huu wa kuogelea nimefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa, nina uwezo wakula mara tatu kwa siku pamoja kuwasomesha Watoto wangu licha ya kwamba nina mume lakini mimi ndio nakuwa mchango mkubwa zaidi katika familia yetu” Kaije Said Bakar kinara wa mchezo wa kuogelea Tumbe Pemba
Licha kipaji cha kuogelea alichobarikiwa Kaije
alisema suala la kutokuwepo kwa mashindano na mabonanza ya kuogelea ya kila
mwaka pampoja na kukosekana kwa klabu zinazosimamia mchezo wa kuogelea Kisiwani
Pemba ni jambo linalomkosesha usingizi kila uchao kwani alisema kukosekana kwa
mambo kunawafanya wanawake wenye vipaji vya kuogelea kutokupata hamasa ya
kuendelea na mchezo huo, hivyo ameomba wadau wa michezo kuanzisha klabu maalumu
itakayosimamia na kuanzisha mashindano ya kuogelea kwa wanawake.
Alisema “kwakweli waogeleaji wanawake
wa Pemba tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa klabu maalumu
zinazotusimamia na kukosekana kwa mashindano yatakayotuwezesha kuonesha vipaji
vyetu ili tuweze kutambulika na kujipatia kipato”
Mize Hamad Sadiki na Fatma Hamad Ali
ni miongoni mwa wanafunzi wa Bi. Kaije walisema mafunzo ya siku kumi tano
yalitosha kumuwezesha kuwa na uwezo mzuri wa kuogelea na sasa wanaendelea na
shughuli zao za upandaji wa mwani katika kina nirefu cha maji pamoja na
kushiriki katika mashindano ya kuogelea na kuibuka washindi.
“Bi. Kaije kwetu tunamuona kama
mwanamke wa mfano katika jamii yetu ya Tumbe mashariki kutokana na kujitoa
kwake kutusaidia wanawake wenzake kutufundisha kuogelea hadi kufikia kiwango na
sisi kuwafundisha wenzetu, kufanya shughuli zetu za upandaji wa mwani katika
kina kirefu pamoja kushiriki mashindo yaliyoandaliwa na taasisi ya Milele
Zanzibar Foundation na kupata zawadi sio jambo dogo kwetu” walisema
Lakini licha uwezo na kipaji kizuri cha kupasua Bahari (kuogelea) alichojaaliwa Kaije, alisema anakabiliwa na ombwe la simanzi kwa kutokuwepo kwa mashindano maalum ya mchezo wa kuogelea ili kuonesha uwezo wake, kutambulika na kujipatia kipato, na kuwaomba wadau na taasisi husika za Serikali kuanzisha mashindano hayo alau kwa mwaka mara moja ili kukuza vipaji vya wanawake kwenye mchezo wa kuogelea Kisiwani Pemba.
Sio wanaume wengi katika jamii zetu
wanaowaunga mkono wake zao wanapofanya vitu vya tofauti kama ilivyozoeleka
lakini kwa upande wa bwana Mwinyi Ali Mussa ambaye ni mume Gwiji wa kuogelea
Tumbe Mashariki Kaije Said Bakar, alisema kwake ni fahari kuona mke wake ni
kiongozi kwa wanawake wenzake kwenye mchezo wa kuogelea kwani umemsaidia kwa
kiasi kikubwa kujikwamua kimaisha pamoja na kutoa elimu ya kuogelea kwa
wanawake wenzake na hata wanaume.
Alisema “Unajua kazi ni kazi za Bahari kwahivyo kujua kuogelea ni jambo muhimu sana sio kwa wanaume wala wanawake kwahivyo mke wangu kuwa na uwezo mzuri wa kuogelea kiasi ya kuwafundisha wanawake wenzake pamoja na kushiriki warsha mbali mbali kupitia mchezo wa kuogelea kwangu ni fahari na sio kwangu tu hata kwa jamii ya Tumbe kwa ujumla”






Comments
Post a Comment