Na, Hassan Msellem, Pemba
Suala la ubaguzi wa Kijinsia kwenye michezo maskulini ni moja miongoni mwa sababu zinazopelekea wanafunzi wakike kutoshirikishwa kwenye baadhi ya michezo ikiwemo mpira wa miguu.
Hayo yamedhihirishwa na wanafunzi wakike na walimu kwenye Skuli mbali mbali Kisiwani Pemba, wakati mwandishi wa Habari hizi alipofanya mahojiano na walimu na wanafunzi juu ya suala la usawa wa Kijinsia kwenye michezo maskulini.
Hajra Jabir Suleiman na Nadra Juma Rajab ni wanafunzi wa Skuli ya msingi Michakaini Chake Chake Chake Pemba ambao wanashiriki michezo mbali mbali skulini hapo wamelalamikia suala la kubaguliwa kwenye michezo kama vile mpira wa miguu kwa kisingizio cha jinsi yao ya kike huku mchezo huo ukinasibishwa na Vijana wakiume pekee.
"Licha ya kucheza Netball na Nage lakini napenda kucheza mpira wa miguu pia ila kila ninapomuambia Mwalimu wa michezo ananikatalia anasema wanawake haturuhusiwi kucheza mpira" alisema Hajra
"Mwanzo nilikuwa napenda kuangalia wanaume wakicheza mpira nami nikavitiwa na kucheza mpira lakini nilipomuambia mwalimu akasema uwanjani nitakuwa mwanamke peke yangu itakuwa sio vizuri" Nadra Juma Rajab
Habiba Juma Jafar ni mwalimu wa somo la michezo Skuli ya msingi Michakaini, alisema kutokuwepo kwa mazingira mazuri ya kimichezo katika skuli hiyo ni moja miongoni mwa sababu zinazowakosesha nafasi wanafunzi wa kike kushiriki kwenye baadhi ya michezo ikiwemo mpira wa miguu.
"Sio kwamba tunawakataza wanafunzi wakike kushiriki katika michezo wanayocheza wanaume ikiwemo mpira wa miguu lakini ukiangalia kwanza wanafunzi wenyewe wakike sio wengi wanaopenda kucheza mpira lakini hata hao wachache waliopo tuna shida ya eneo la kuchezea maana ukiangalia tulikuwa na Uwanja lakini eneo Hilo kwasasa linajengwa na Skuli yetu Haina eneo kubwa la wazi, lakini hata baadhi ya walimu hawako tayari kuwaruhusu wanafunzi wakike kushiriki kucheza mpira kutokana na Mila na desturi zetu" alisema



Comments
Post a Comment