Na, Thuwaiba Habibu
Raha na furaha ya safari ni kufika ulikokusudia kwa salama na amani.
Baadhi ya safari huwa ngumi na huwa zenye maumivu na athari nyingi
Miogoni mwa safari hizi ni ya waandishi wa habari kutaka kuwa na sheria zenye mazingira bora ya kazi zao.
Kwa Takribani miaka 20 sasa waandishi na wadau wengine wa habari wamekuwa wakionyesha vifungu vya sheria ya habri vinavyominya uhuru wa habari na wa kujieleza.
Lengo ni kutaka sheria rafiki itakayofanya mazingira ya kukusanya na kutoa habari Zanzibar kuwa rafiki na kuweza kuchangia vizuri maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Lakini kelele hizo zimekuwa kama zile za msemo maarufu wa Kiswahili wa kelele za mpangaji hazimzuwii mwenye nyumba kulala.
Zanzibar ilikuwa na historia nzuri na ya kuvutia ya habari na vijana wake kuchangia maendeleo ya sekta ya habri, hasa ya kufungua idhaa za Kiswahili katika nchi mbali mbali duniani.
Kutoka zama hizo na hadi leo visiwa hivi vimetoa manguli wa taaluma ya habari kwa nyakati mbali mbali.
Ni kwa kuwa na sheria ya habari rafiki ndio Zanzibar inaweza kurejesha hadhi na heshima yake na kutoa nafasi kwa waandishi wa kizazi cha hivi sasa na baadaye kuweza kuonyesha uwezo wao mkubwa wa kuelimisha jamii, kukosoa na kuishauri serikali, pamoja kupelekea sauti za wanyonge na watu wanaodai hawakutendewa haki kusikika.
Sheria nzuri za habari zitapelekea kuondokana na mwenendo wa sasa wa kutoa habari za huyu kasema, Yule kapongoza na mwengine katoa wito.
Badala yake zitasaidia kuibua masuala muhimu yayoigusa jamii na watu kuweza kuelewa serikali yao inafanya nini, bali hata kuiambia serikali wanataka nini.
Hii ikiwa na pamoja na kueleza wanataka vitu gani vipewe umhimu.
Kwa sasa vyombo vya habari vya Zanzibar haviwapi watu wanachokitaka na umma umekuwa ukipokea salamu tu za viongozi, lakini watu hawana nafasi ya kutosha ya wao kuwaambia viongozi wanachotaka au kuishauri serikali yao
Kwa muhtasari, waandishi wa habari wa Zanzibar wamekuwa kama matarishi wa kupeleka ujumbe kutoka kwa viongozi kwenda kwa wananchi na sio kuchukua salamu za wananchi kwenda kwa viongozi.
Mingoni mwa sheria zinazolalamiki kuwa zinawabana mbavu na koo waandishi wa habari wanaofanya kazi Zanzibar ni za Baraza la Wawakilishi, uchaguzi na ya mitandao. Sheria hizi zinahitaji kupigwa tochi ili ziwe na mazingira rafiki kwa waandishi wa habari.
Kuwepo kwa sheria hizi kumepelekea ulinzi wa waandishi wa habri kuwa hatarini na hii imethibitika kwa waandishi kupigwa marufuku , kupigwa kunyang’anywa vifaa vya kazi, kufunguliwa mashitaka bandia na baadhi ya vituo vya radio na magazeti kufungiwa.
Kwa mfano, panapotokea mwalimu wa skuli kufanya makosa hatuoni skuli kufungwa bali mwalimu aliyeenda kosa kuwajibishwa kisheria na hivyo hivyo daktari au muuguzi akikosa kufuata maadili huwajibishwa yeye na sio kufunga hospitali.
Lakini mwandishi akionekana labda ameipotosha umma au kafanya kosa utaona chombo chake kinaadhibiwa na hata kufungwa.
Tujiulize hivyo hii ni haki au uonevu kwa kutumia sheria ambazo nikandamizi?
Kwa kuwa na sheria ngumu na hatarishi kazi ya uwandishi wa habari Zanzibar imekuwa ngumu na hata kupelekea waandishi kutoweza kufuatilia habari ambazo wananchi wanataka ukweli wake.
Katika kila nchi waandishi wa habari sio tu mawakala wa kuleta mabadiliko ya kheri bali pia ndio sauti ya wanyonge. Sasa kama waanadishi wanatarajiwa kuzisikiliza sauti za wanyongwe, wamefungwa midomo na wananyang’anywa vifaa vyao vya kazi wataweza kuifanya kazi hii?
Hii ndio inayopelekea wananchi, kama wale ambao ardhi na mashamba yao kuporwa, kubaki wanalia na hawana wa kuwanyamaza.
Mtu akiibiwa hupeleka malalamiko yake polisi na uchunguzi hufanyika kumpata mhalifu, lakini watu wakiwa na malalamiko ya kukosa maji au huduma kuwa mbovu katika kituo cha afya hawawezi kwenda polisi kuweka riporti.
Kimbilio lao huwa kwa vyombo vya habari na kama waandishi mikono imefungwa pingu na midomo imefungwa wananchi watabaki kulalamika pembeni na sauti zao hazisikiki.
Wazo la kufanyanyiwa marekebisho ya sheria za habari limeshawahi kutolewa maelezo kuwa ndio nyezo itakayo fanya wanahabari kuwa na hamu ya kutoa taarifa zilizo na mvuto zaidi kutokana na baadhi ya wadau kuviorozesha vifungu visivyotoa fursa kwa waandishi kuteleza wajibu wao ipasavyo.
Wadau wa habari wanaonekana kuchoshwa na ahadi za serikali za kila siku kuambiwa zoezi la kurekebisha sheria za habari na kujieleza zipo mbioni.
Sasa ni zaidi ya miaka 20 tokea kusikika kuanza kwa hizo mbio. Ni vizuri hizo mbio zikafikia kwenye mfundo ili twende na wakati.
Ni kweli maneno matamu humtoa nyoka pangoni, lakini akitoka hutarajia hio ahadi aliopewa anaiona baada ya kutoka pangoni.
Kwani maneno mengine matamu hayamshibishi mtoto mwenye njaa anayetaka kunyonya
Anachohitaji ni chakula na sio maneno mazuri au kupakwa uturi.
Mwisho.

Comments
Post a Comment