Na, Ahmed Abdalla, Zanzibar.
WANAWAKE nchini wametakiwa kuhamasishana kuepuka vishawishi vya rushwa ya ngono ili kuwa imara na jasiri wanapotaka kugombea nafasi za uongozi.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa uhusiano kutoka Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA), Mwanaidi Suleiman Ali alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya mwanamke katika kupambana na rushwa ya ngono katika uchaguzi, katika mafunzo kwa wagombea watarajiwa yaliyofanyika ofisi za TAMWA Zanzibar Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.
Alisema ana imani kwamba wanawake wengi wanaweza kupambana na rushwa ya ngono hivyo ni vyema kuhamasishana ili kuona kila mmoja anakuwa imara na anaweza kukabiliana na hali hiyo.
Ofisa huyo alifahamisha kuwa wapo baadhi ya wanaume huutumia mwanya huo ili kuwakatisha moyo na kurudisha nyuma jitihada zao hivyo ni vyema kukitokezea kitu kama hicho kujitathmini na kuwaimara katika kukabiliana nayo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Uzoefu unaonesha kwamba wanawake waathirika wakubwa wa matukio hayo sio katika masuala ya kisiasa tuu bali hata katika masuala mengine ikiwemo ya kiuchumi wamekuwa wakirudishwa nyuma na kushindwa kufikia malengo yao,alisema.
Baadhi ya wanawake wa vyama vya siasa wamesema sasa wanapaswa kushirikiana katika mapambano ya rushwa ya ngono ili kutimiza malengo yao ya kuwa viongozi bila ya madhara.
Walisema hakuna sababu za msingi ambazo zinamkataza mwanamke asigombee nafasi mbalimbali za uongozi ila kilichokuwepo ni miundombinu ya kurudisha nyuma jitihada za wanawake katika kushika nafasi hizo.
Walisema umefika wakati sasa kwa wanawake kusimamaimara na kuwa mabalozi katika kuelimishana juu ya suala hilo ili wakati unapofika kuweza kujiepusha na matukio hayo.
Kwa mujibu wa mamlaka ya kuzuia, rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ZAECA waathirika wakubwa wa rushwa ya ngono katika chaguzi ni wanawake na baadhi yao kushindwa kukabiliana nayo na kupelekea athari mbalimbali katika maisha yao ya kisiasa.
Mkutano huo umeandaliwa na tamwa ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi (SWIL), unaotekelezwa kwa pamoja na TAMWAZNZ, ZAFELA na PEGAO ambao unafadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

Comments
Post a Comment