ZANZIBAR.
Na Nafda Hindi.
Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari Tanzania TAMWA ZNZ Dk Mzuri Issa amesema kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini kutarahisisha maendeleo ya haraka kwa Taifa.
Dk Mzuri ameyasema hayo katika mkutano wa kujadili mapungufu ya sheria zinazokwamisha uhuru wa habari Zanzibar uliwashirikisha watendaji kutoka Wizara ya Habari.Utamaduni,Utalii na Vijana, Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Tume ya Utangazaji, Kamati ya vyombo vya Habari Zanzibar (ZAMECO) na waandishi wahabari uliofanyika Ofisis za TAMWA Tunguu Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akitolea mfano wa nchi zilizopiga hatua kimaendeleo kama Marekani na kwa Afrika ni pamoja na Afrika ya Kusini na Mozambik kwa kuvitumia vyema vyombo vya habari vimesababisha kuinua uchumi wa nchi hizo na kuleta mabadiliko.
“Nchi yetu ina Amani na maendeleo ya kiuchumi lakini suala la uhuru wa habari ni jambo muhimu na tuna wajibu sisi wadau kuhakikisha unafikiwa na kutelelezwa ipasavyo, Dk Mzuri Issa.
Aidha amesema pamoja na kuridhia Mikataba ya Kimataifa na Kikanda bado Tanzania sauti za wananchi hazipewi kipau mbele kusikika katika vyombo vya habari ukilinganisha na sauti za Viongozi jambo ambalo linawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni yao.
“ Sheria, Kanuni na Sera ndizo zinazotowa mustakabal mzuri watu kuripoti habari endapo tutakuwa na sheria zisizo rafiki habari itakuwa ni ngumu kuripotika na kusababisha kukosa kasi ya maendeleo, Dk Mzuri Issa.
Mapema Afisa mradi wa Uhuru wa Habari kutoka TAMWA ZNZ Zaina Mzee amesema sauti za wananchi zipewe nafasi ya kusikika kupitia vyombo vya habari kwa lengo la kupata maendeleo nchini.
Akiwasilisha mada inayohusu Mapungufu ya Sheria ya habari Mwandishi mwandamizi Hawra Shamte amesema ingawa kuna sheria zinazosimamia sekta ya habari bado zinaonekana kiuhalisia hazifanyi kazi ipasavyo kwa kulinda Usalama wa waandishi wa habari na wananchi hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho.
“Mikataba mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa inalinda tasnia ya habari, waandishi wahabari na watetezi wa haki za binadamu na kulinda wajibu wa Serikali kufuata, kuendeleza uhuru wa kutoa maoni na kujieleza, Hawra Shamte.
Mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Kimataifa la haki za binadamu (Universal Diclaration) na mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCR) ambayo Tanzania ni moja ya nchi iliyoridhia mikataba hiyo, ambapo nchi mia moja na sabiini na mbili (172) zimeridhia mkataba wa haki za kiraia na kisiasa.
Mkataba mwengine ni mkataba wa Bara la Afrika unaojuilikana kama mkataba wa haki za binadamu na haki za watu wa Umoja wa Afrika, uliopitishwa mwaka 1981 (Afrika Charter on Human Peoples Right) ulianza kutumika (1986) na mkataba huo hadi kufikia mwaka (2002) tayari ulisainiwa na nchi mia moja hamsini na tatu (153) za Afrika.
Bi Hawra akizitaja sheria hizo amesema ni pamoja na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu no 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 (1997) iliyofanyiwa marekebisho na sheria no 1 (2010).
Afisa Sheria kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mwanaid Juma Suleiman amesema Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu no 5 (1988) iliyofanyiwa marekebisho na Sheria no 8 (1997) kwa vile mchakato wake ni wa muda mrefu tayari imeshapita katika maoni ya wadau na sasa ipo katika hatua ya makatibu wakuu kufanyiwa marekebisho mbali mbali.
Afisa huyo amesema kwa upande wa Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 (1997) iliyofanyiwa marekebisho na sheria no 1 (2010) Wizara husika haijapokea Sheria hiyo na kwa sasa Tume ya Utangazaji Zanzibar ndio inayoshughulikia sheria hiyo.
Sheria hiyo ilisitishwa kuendelea na mchakato wake kwa sababu kanuni na sheria zilikuwa tofauti na inabidi hadi kufanyiwa marekebisho ziendane, na mpaka sasa hivi Wizara haijapokea sheria hiyo,ila itakapokuja basi tutashughulika nayo haraka iwezekanavyo, Afisa sheria Wizara ya Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo.
Nae Mwanasheria kutoka Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar Sabra Mahmoud Iddi amesema wanategemea mchakato wa Sheria ya habari utafanyiwa marekebisho ili kupata sheria bora zinazozingatia maslahi ya waandishi na uhuru wa vyombo vya habari.
“ Marekebisho ya sheria ni mchakato wa muda mreu unaopitia ngazi hadi ngazi ili kupata sheria bora, hivyo amewaomba waandishi pamoja na wananchi kuwa na subra kwa lengo la kupata sheria bora zinazokwenda na wakati. Mwanasheria, Tume ya kurekebisha Sheria.
Salim Said Salim ni mwandishi mkongwe amesema Zanzibar waandishi wanakutana na vikwazo mbali mbali wanapokuwa katika kutekeleza majukumu yao na hata vyombo vya habari hufikia hatua ya kufungiwa kutokuendelea na kazi zao za utangazaji.
Matukio kama haya Zanzibar yako mengi kufungiwa ovyo kwa vyombo vya habari na hata waandishi wanaekewa vikwazo ikiwemo kunyanganywa vitambulisho vyao vya kufanyia kazi hatua hii inawanyima wananchi kupata habari, Salim Said Salim.
Jabir Idrisa mwandishi wahabari amesema Enzi za utawala wa Kisultan Zanzibar kulikuwa na magazeti Zaidi ya 50 ukilinganisha na hali iliopo sasa kuna gazeti moja pekee linalomilikiwa na Serikali hivyo marekebisho ya sheria yanahitajika ili kutoa nafasi kwa raia kumiliki magazeti binafsi.
Nao waandishi wahabari wamesema wanakutana na vikwazo kadhaa katika kufanikisha majukumu yao na kutowajibika ipasavyo kwa kuhofia usalama wao wakati hakuna sheria yoyote inayowalinda endapo watapatwa na tatizo.
MWISHO




Comments
Post a Comment