Salhida “ndoto yangu ni kuwa kiongozi na kuleta mabadiliko”
Anzia nafasi ya Makamu wa rais Serikali ya wanafunzi Pindua Pemba
Wazazi wake, majirani, wamtaja mwenye kuona mbali
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
SALHIDA Amour Rashid mwenye miaka 18, ni miongoni mwa vijana wa kike wenye ndoto za kufika mbali katika suala la uongozi.
Kwa sasa yupo wa kidato cha nne katika skuli ya Sekondari ya Mohamed Juma Pindua wilaya ya Mkoani Pemba.
Akiwa skuli hapo kijana huyo, anaitumikia nafasi ya Makamu wa Rais katika serikali ya wanafunzi skulini hapo.
"Ukiwa na malengo fulani katika maisha, ni lazima kutakuwa na vitu vingi vizuri, vikija utakuwa na hamu ya kuvifikia, lakini ikiwa sio kiongozi sio rahisi,’’anasema Salhida.
Skuli ya sekondari ya Mohamed Juma Pindua ina wanafunzi 969 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, huku serikali ya wanafunzi ikiwa na viongozi 14, wakiwemo wanawake wanne na wanaume 10.
Akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano waliozaliwa katika kijiji cha Kidini Mkanyageni wilaya ya Mkoani Pemba.
Kilichomshawishi Salhida, kugombea uongozi ni kutokana na malengo aliyojiwekea, katika maisha yake na hivyo kuamini kuwa, atakapokuwa kiongozi anaweza kuyatimiza haraka malengo yake.
"Uongozi upo kwenye damu yangu, hivyo nikaona na mimi nigombee, kwa sababu nitapata nafasi ya kusaidia kutatua changamoto zinazotukabili skuli, na pia nitajijengea uthubutu na ujasiri popote nitakapokwenda," anasema wakati akiwa nyumbani kwao.
Mwanafunzi huyo anasema, atakapomaliza kusoma elimu ya lazima na chuo kikuu, anatarajia kuingia kwenye mchakato wa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Lengo lake ni kuhakikisha, anaingia kwenye vyombo vya maamuzi na kuweza kuwatetea wanawake, katika mambo yanayowahusu pamoja na kuwaletea maendeleo wanajamii kwa ujumla.
Tulimpa ushirikiano Khadija Salim mama mzazi wa mtoto Salhida anasema, walipopata taarifa ya kwamba, binti yao anagombea nafasi ya uongozi wa skuli, walimpa ushirikiano ili afanikishe ndoto yake.
"Sisi tulimpa ushirikiano mtoto wetu, kwa kitu ambacho amekipenda na nilipopata taarifa ya kuwa amefanikiwa kuchaguliwa nafasi hiyo, nilipata faraja," anaelezea mama Salhida.
Nguvu ya kushinda kwenye ngazi ya uongozi kwa Salhida inatoka pia kwa baba yake Amour Rashid, anakiri kuwa walimuandaa kwa malezi mazuri mtoto wao, na kumpa maelekezo zaidi kuwa yeye katika familia ni wa kwanza.
"Nilimwambia yeye tayari ni kiongozi kwa sababu amezaliwa wa kwanza katika familia, kwa hiyo ajipange kuwa ni mfano mzuri kwa ndugu zake, licha ya uongozi huo wa kuchaguliwa," anasema Amour.
Amour ameongeza kwa kusema kuwa, kuwadharau wanawake kuwa hawafai kuwa viongozi, si jambo zuri kwani, wakiwezeshwa wanaweza na wanaleta mabadiliko chanya katika nafasi zao.
Maendeleo ya Elimu
Mwalimu Mkuu wa skuli ya Mohamed Juma Pindua, Ali Simai Makame amuelezea Salhida kuwa, ni mwanafunzi anayependa masomo yake na anafaulu vizuri, hivyo kuwa kiongozi kutamsaidia kukua kiakili zaidi.
"Serikali ya wanafunzi inawaandaa watoto kuwa viongozi wazuri na kuwajengea uthubutu, kujiamini hasa kwa wanawake, ambao kwa muda mrefu wameachwa nyuma katika masuala ya uongozi," anafafanua.
Anasema, Salhida ni mwanafunzi mwenye nidhamu, anaejituma na ana uwezo mzuri wa kujieleza, hivyo ni kiunganishi kizuri, baina ya wanafunzi na walimu.
Akiwa anamzungumzia Salhida, mwanafunzi Saida Salum Nassor anasema kuwa, ana kipaji cha kuongea tangu zamani, hivyo kuingia katika uongozi, kutamsaidia sana kukuza kipaji chake.
"Kila kitu kina mwanzo, kwa hiyo naamini kuwa kuwepo katika serikali ya wanafunzi, kutamjenga kujiamini zaidi na mwisho wa siku atagombea nafasi nyingine, ikiwemo za majimboni," anaeleza.
Waliomzunguka
Kwa upande wa majirani zake Salhida, akiwemo Asha Hassan anaeleza, amekuwa na kawaida ya kuwa shughulikia wadogo zake, hivyo waliposikia amepata nafasi ya uongozi, hawakushangaa.
”Salhida muonekano wake unakuambia kuwa ni mtoto anaeweza kuwa kiongozi, kwa sababu ni mtoto anaejiamini na anaweza kuongea," anasema Sakina Hamad Iddi.
Safari na ndoto
"Waliniambia ninachostahili kufanya kilicho chema basi nifanye, wala nisisikilize maneno ya watu, muhimu nifanye wajibu wangu unaotakiwa, kwa kufuata maadili mema," anasema Salhida.
Wito wake ni kuwa anawashauri watoto wenzake, waamini kwamba kuingia katika uongozi ni kuanza kujitengenezea maisha mazuri ya baadae, hivyo wasiogope bali wanapaswa kuamua tu kwa sababu wanaweza.
"Nawashauri wajiingize katika uongozi kwani ni moja ya njia ambayo itawasaidia katika kazi na maendeleo ya baadae katika maisha yao," anamaliza Salhida.
Wanaharakti wanasemaje?
Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa PEGAO Pemba anasema kuwa, mtoto anapoanza mapema harakati za uongozi, anakuwa vizuri katika kila hatua kwani huwa upo kwenye damu yake.
"Uongozi ni kipaji na ndio mana mwanamke mwenye ndoto za uongozi anaanza mapema tangu akiwa skuli, hivyo hivi vipaji tunatakiwa kuviendeleza ili wasirudi nyuma," anasema.
Afisa Mkuu wa Mahusiano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Safia Ngalapi anasema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu ya uongozi kwenye jamii ili kusudi waelewe kila mmoja ana haki ya kushiriki katika uongozi na wanawake wanapata nafasi ya kuingia kwenye vyombo vya maamuzi.
Anasema, jamii inahitaji kuwakubali watoto wenye vipaji vya kuongoza ili watakapokuwa wakubwa, iwe ni rahisi kuingia majimboni kugombea uongozi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment