"VITISHO VISIWE SABABU YA KUTOKUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI" MKURUGENZI TAMWA, ZNZ
Na, Thuwaiba Habibu
Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar Dkt Mzuri Issa Ali amewataka wanawake kutokuogooa vitisho kutoka kwa mtu yoyote ili kuweza kupambania ndoto zao za kuwa viongozi .
Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa mkutano Tunguu,Unguja katika kikao na wadau mbali mbali kujadili namna gani wanawake wanapata ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia mitandaoni
Alisema kuwepo kwa vitisho kumewafanya wanawake kuacha kugombe ikiwemo kukatazwa, kuvunjwa moyo, kukemewa na tuhuma kutoka mitandaoni ambazo bado zina wadhalilisha na kurejesha nyuma juhudi zao katika kugombea.
"Wanaume hutumia uongo kumchafua mwanamke kwasababu jamii inaamini yeye ni mtu ambaye atakiwi kuwa na doa basi ni rahisi kumkosesha."
Kwa upande wake Afisa Sheria Mwandamizi wa Vyama Vya Siasa Abdul razak Said Ali amesema kuwepo kwa asilimia 50 baina ya wanawake na wanaume ni harakati za muda mrefu na sasa zinaendelea ili kuwe na uwiano sawa.
Alisema kupitia tamko la jumuiya ya Maendeleo la Nchi za kusini mwa Afrika( SADC) la mwaka 2005 na itifaki ya maendeleo ya jinsia 2008 imetekeleza kiwango cha chini cha ushiriki wa wanawake kwa 30%na baadae kuimarishwa hadi 50%
Aidha alisema changamoto ya uchumi ni kikwazo kwa wanawake katika shughuli za kisiasa ni lazima kila chama kitenge bajeti itakayowezesha wanawake kufikia malengo yao.
"Mfumo wa uteuzi katika vyama vya siasa unaathiriwa kwa kiasi kikubwa na ule wa kifedha ambapo wanawake wengi hukosa fursa," alieleza abdul razak.
Nae Afisa kutoka Malaka ya kupambana na rushwa na Uhujumi uchumi Zanzibar (ZAECA) Yussuf Juma Suleiman amesema moja ya sababu ambazo zinawakwamisha wanawake katika kugombea nafasi za uongozi ni rushwa ya ngono
Amesema kuwa, kabla wanawake hawajaingia katika kugombea nafasi za uongozi, ni vizuri kupewa elimu ya uraia, ili kujua miiko na misingi ya uongozi, ili wasiwe na mwanya wa kutoa rushwa.
Aidha amesema kuwa, serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepitisha sheria mpya ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi, sheria namba 5 ya mwaka 2023, kifungu cha 53.
Amesema, kifungu hicho kimeharamisha rushwa ya ngono, kwa kukataza mtu yoyote kushawishi, kuahidi kufanya ngono na adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka saba na kisichozidi miaka 10
“Rushwa ya ngono ni uhalifu kama ulivyo mwingine, na serikali imeazisha sheria ili kukabiliana nayo, lakini wandishi wa habari toeni elimu ili wanawake wanaotia nia wasiwe ni mwanya wa kutokea rushwa,’’ alisema.
Nae mdau Mwatima Issa, Rashid alisema kila mtu anatakiwa akipe tamani kitu anachofanya ili kufikia malengo aliojiwekea kwani ukiwa unajikubali utafika mbali.
Comments
Post a Comment