SERA YA WATU WENYE ULEMAVU BADO NI KIZUNGUMKUTI KWA WANAWAKE WENYE ULEMAVU PEMBA.

 Na, Hassan Msellem-Pemba

“Ndoto yangu ni kuwa Mbunge au Mwakilishi ili niwatetee wenzangu wenye ulemavu kama mimi lakini ndoto hiyo inashindwa kukamilika kutokana na mfumi wa vyama vyetu vya siasa dhidi ya watu wenye ulemavu” Amesema Hidaya Abedi Khamis mwenye ulemavu wa viungo anayeishi Shehia ya Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Hidaya mama wa watoto watatu na Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) na Afisa Watoto Wenye Ulemavu Wilaya ya Chake Chake na mfuasi wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwa miaka 25 sasa.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Sura ya Tatu Ibara ya 11. (a) inaeleza kuwa watu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, Sheria ya watu wenye Ulemavu za Zanzibar ya nambari 8 ya mwaka 2022 na Sera ya Watu wenye ulemavu Zanzibar ya mwaka 2018 pamoja na Mikataba mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa, imeweka sawa suala la  usawa kibinadamu licha ya mapungufu walionayo bado mifumo katika vyama vyote vya siasa nchini havijatoa fursa sawa kati ya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

“Mwaka 2010 nilichukua fomu ya kugombea nafasi ya uakilishi katika Jimbo langu la Ole Wilaya ya Chake Chake,Mkoa wa Kusini Pemba,baada ya baadhi ya wanachama kunishawishi kufanya hivyo” Amesema Hidaya huku akiongezea kuwa ushawishi huo ulimpa moyo wa uthubutu na kuchungua fomu baada ya kuona uwezo wangu nami nikafanya hivyo “ Nilishangaa kuona viongozi wa chama waliposikia tu nimechukua fomu wakaanza kuzungumza maneno mabaya sana dhidi yangu na hatimaye sikupendekezwa kuwa mgombea ila sikukata tamaa mwaka 2020 nikagombea nafasi ya Udiwani” Amesema Hidaya.

Ambaye alipata nafasi ya kuwa mshindi wa watatu lakini kwa mazingira magumu mno na maneno ya dhihaka juu yake.

Watu wenye Ulemevu wanapaswa kupata haki zote wanazopata wale wasio na Ulemavu ikiwemo haki ya kuishi, kuthaminiwa, kupendwa, kupata elimu pamoja haki ya kufanya kazi kwenye taasisi binafsi na pia kuchanguliwa kuwe viongozi.

Hali halisi

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya wakaazi Zanzibar 1,889,773 ambapo kati ya hao Watu 215,434 ni watu wenye Ulemavu ambapo ni sawa asilimia 11.4.

Taarifa za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ya mwaka 2023 (Zanzibar Statuctics Abstract) inaonesha kuwa  Zanzibar ina jumla ya watu wenye ulemavu kuanzia miaka 0 hadi 65 ni 8,100 huku kuanzia miaka 15 hadi 65 ni 6,843.

Udhaifu wa Kiutendaji na Ulemavu ni vitu viwili tofauti, wapo viongozi ambao hawana ulemavu lakini hawana sifa za kuwa viongozi lakini wapo Viongozi Wanawake wenye Ulemavu ambao ni wakupigiwa mfano katika Taifa kama vile Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Abeda Rashid Abdalla, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Anna Atanas pamoja na Mbunge wa Viti Maalum ambaye alikuwa msanii wa kizazi kipya Khadija Taya (Keisha).

Aisha Ali Abdalla 28, ni mwenye ulemavu wa uoni ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya Wasioona Wilaya ya Chake Chake Pemba, amewahi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza  la Vijana Wilaya ya Chake Chake kwa mihula mitatu mfululizo lakini ameshindwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kwa kile anachodhani kukosa elimu ya mafunzo ya uongozi na pili kutokana na hali ya ulemavu aliyonayo inamkosesha fursa hio. “Sijawahi kupata mafunzo yoyote kuhusu uongozi kiasi kwamba mpaka nakwenda kwenye kiriri cha kuomba kura sifahamu lolote kuhusu majukumu haswa ya nafasi hiyo lakini pia hata mazingira hayakuwa mepesi kwangu katika harakati za kampeni kwasababu nilikuwa sikuwa na mtu wa kunishika mkono” Amesema Aisha.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Yusuf Juma Ali, amekiri kuwa Katiba ya CCM, haijaweka wazi mazingira rafiki ya watu wenye Ulemavu kwa watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi za uongozi na kuibuka kidedea licha kupata fursa ya kuwa wanachama. “Kila mwenye umri kuanzia miaka 18 wanaruhusiwa kujiunga na chama bila ya kuangalia hali yake kwa hivyo hata hao watu wenye ulemavu wamo kwenye chama na wanaruhusiwa kugombea nafasi yoyote wanayopenda kama wanachama” Juma ameendelea kusema kuwa  “Ingawa Katiba haikuwaeleza moja kwa moja ila suala la kuomba ridhaa ya chama kugombea na kushinda itategemea na mtu mwenye anavyokubalika kwenye chama” Amemaliza.

Katiba ya Chama Cha ACT Wazalendo haikutofautiana na Katiba ya CCM kwani katika Sura Ibara ya 8. (1) inayozungumzia UANACHAMA NA UONGOZI imesema Uanachama wa ACT utakuwa wazi kwa raia wote wenye umri wa kupiga kura bila kubagua jinsi, kabila, dini na hali yoyote.Hamad Shavuai Suleiman ni Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Kaskazini Pemba, amesema “Chama cha ACT Wazalendo ni chama kinachoongoza kwa kuwapa nafasi watu wa makundi yote wakiwemo watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake na Wazee” Ameendelea kusema kuwa “Watu wenye ulemavu hajawaacha nyuma kwenye Katiba yetu ni wao wenyewe tu kuamua kujiunga na chama na kugombea nafasi mbali mbali za uongoni” Amemalizia.

Maoni ya wananchi mbalimbali yote yamesimama juu ya mstari mmoja kuwa wanawake wenye Ulemavu bado hawajapewa nafasi sawa kama wanawake  wengine katika nyanya zote licha kuwepo kwa Sheria, Sera zenye maelezo mazuri kuhusu usawa watu wenye ulemavu.

Mariam Juma Faki 45, Mkaazi wa Mkoroshoni Chake Chake na mjasiriamali wa biashara ndogo ndogo amesema “Hizo Sheria na Sera zimetengenezwa tu ili kuwafariji watu wenye ulemavu lakini bado watu wenye ulemavu wanapitia changamoto nyingi sana na upande wa kugombea uongozi” Amemaliza Mariam kutoa maoni.

Hidaya anamalizia kwa kusema kuwa “Bado vyama vya siasa na jamii haijatuona kuwa watu wenye ulemavu tuna haki sawa na tunaweza kuwa iongozi na kuleta mabadiliko” Amemalizia Hidaya.

 

Comments

Popular posts from this blog

MWALIMU WA MADRASA MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE

Mama ajifungua kisha kukiua kichanga na kukifukia kwenye tuta- Sizini Pemba

Mtangazaji wa Wasafi Media, Dida Afariki Dunia