"MDIPAO" YATOA ELIMU YA UDHALILISHAJI NA MIGOGORO YA ARDHI, MICHENZANI.
Wananchi wa Shehia ya Michenzani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, wametakiwa kuachana na tabia ya muhali na badala yake kuviripoti vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa Kijinsia ili kupambana na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Mkoani (MDIPAO) Hakim Nassor huko Michenzani katika Mkutano kati ya Wasaidizi wa Sheria wa Jumuiya hiyo na Wananchi, amesema miongoni mwa sababu kukoma kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa Kijinsia katika jamii ni muhali pindi vitendo hivyo vinapotokea.
Akiwasilisha mada ya udhalilishaji na ukatili wa Kijinsia Hakimu Mahakama ya Wilaya Mkoani ambaye pia Hakimu dhamana wa Mahakama ya Wilaya Mkoani Suleiman Said Suleiman amewataka Wananchi walioshiriki katika Mkutano huo kutokuwasafisha watoto pindi wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji Ili kusaidia katika ushahidi makosa hayo.
"Tafadhalini sana musiwasafishe watoto wenu pindi wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwani mukiwasafisha munachangia kuondosha ushahidi katika uendeshaji wa makosa hayo" amesema
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo katika Mahakama ya Wilaya Mkoani Nasim Faki Mfaume, amesema miongoni mwa kesi zinazoripotiwa kwa wingi katika Mahakama mbali mbali ni kukithiri ni migogoro ya Ardhi na kuwataka Wananchi kuwa nyaraka sahihi za umiliki wa Ardhi Ili kuepukana na migogoro ya mara kwa mara.
Hakimu Nasim, aliongeza kuwa sababu zinachangia kuongeza kwa migogoro ya Ardhi ni wamiliki na wauzaji kukosa nyaraka halali za umiliki wa Ardhi hali inayosababisha kuibuka kwa migogoro katika jamii
"Utafiti unaonesha migogoro mingi ya Ardhi inasababishwa na wamiliki na wauzaji wa Ardhi kutokuwa na nyaraka halali za umiliki wa maeneo wanayomiliki au kuuza, na hii inasababishwa na wale wamiliki wa mwa zo Yani mababu zetu kutokuwa na nyaraka halali pamoja na kuacha wasia wa kumiliki Ardhi na kutokurithishwa wahusika pindi wazee hao wanapofariki" amesema
Bahati Khamis Sharif 45, na mama wa watoto 6 ni miongoni mwa Wananchi walioshiriki Mkutano huo, ameomba kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya mtoto kwani Sheria hiyo ina mapungufu na inachangia kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa Kijinsia katika jamii.
"Kuna kesi ilitokea hapa mtaani mtoto wakike wa miaka 14 amefanyiwa vitendo vya udhalilishaji na Vijana wakiume wenye miaka 17 kesi ikaenda Mahakamani lakini mwisho wa siku wale Vijana walikiri kutenda makosa wapewa adhabu ya kulipa faini na fidia kwa familia ya muhanga lakini mpaka muda huu nazungumza hawajalipa fidia Wala faini jamani hii ni haki kweli, hebu tupeni ufafanuzi wa jambo kama hili" Bahati Khamis Ali, alihoji
Khatib Ussi Hamad, Rawali miaka 84, amesema kuongeza kwa vitendo viovu katika jamii ni kukosekana kwa malezi ya pamoja.
"Zamani malezi yalikuwa ni ya jamii yote Yani mtoto wangu analelewa na watu wote mtaani akifanya kosa Mzee yeyote anaweza kumrudi na akija nyumbani analia akiulizwa unalilia nini hana majibu mazuri anatandikwa tena mbona tulinyooka vizuri lakini sasa hivi kila mzazi na mtoto wake na ndio kama hivi tunashindwa maana hakuna malezi ya peke yako" alisema
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo Hakimu Mahakama ya Wilaya Mkoani ambaye pia Hakimu dhamana wa Mahakama ya Wilaya Mkoani Suleiman Said, amekiri mapungufu yaliyomo kwenye Sheria ya mtoto kwani adhabu ya kulipa fidia na faini ambazo zinapaswa kulipwa na wazazi hazisaidii katika kuwarekebisha watoto hao
"Sheria hii imesema endapo mtoto atakutwa na hatia ya kosa la udhalilishaji wazazi wake ndio wanapaswa kulipa fidia na faini Sasa shida inatokea wazazi wengi hawalipi hizo fidia na faini na Sheria haijasema kuwa kama hawakulipa washikwe na kuwekwa ndani" alifafanua
Iddi Thani Suleiman, amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili ni kuhidhiwa kwa maeneo mengi ya Ardhi na wawekazaji Hali inayosababisha Wananchi kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao za kila siku
Miongoni mwa hoja iliyoibuliwa ni Dawati la kusikiliza malalamiko dhidi ya Akina Mama na watoto kwamba inachangia kuporomoka maadili ya watoto katika jamii kama anavyosema, Mohammed Ali Mbwa maarufu kwa jina la Zabadi "Sasa Kuna haya madawati ya Akina Mama na watoto nayo yanachangia kwa kiasi Fulani kuharibu maadili yetu maana ukimgusa mtoto unaenda kushitakiwa na mara unafungwa Sasa hatujui hata tufanye nini" alihoji
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo katika Mahakama ya Wilaya Mkoani Nasim Faki Mfaume, amefafanua "Hiyo hoja ipo sana mitaani lakini niseme kwa kimywa kipana hapa kuwa hakuna Mahakama yoyote hapa Zanzibar imewahi kupokea kesi ya aina hiyo kwamba Kuna mzazi ambaye amefunguliwa kesi kwasababu amemuadabisha mtoto kama kwa mujibu wa Sheria ila ukimuhukumu kiasi ya kumjeruhi au kumvunja hapo ndipo unaweza kufunguliwa mashtaka kwasababu umemuathiri badala ya kumuadabisha"
Comments
Post a Comment