MABARAZA YA VIJANA, SIASA NA USHAWISHI SUALA LENYE MAONI TOFAUTI.
Na, Hassan Msellem- Pemba
Historia ya kuanzishwa kwa
Mabaraza ya Vijana ilianza mwaka 1948 katika nchi ya Urusi, ambapo lengo
la kuanzishwa kwa mabaraza hayo ni kuwaunganisha Vijana wa maeneo mbalimbali wa
Taifa hilo ili kutambuana na kuwa wazalendo wa taifa lao,hasa pale inapobidi
kulitetea dhidi ya adui, ikizingatiwa kipindi hicho dunia ilikuwa inakabiliwa
na Vita vikuu vya Pili.
Huko Kisiwani Pemba Katibu Mtendaji wa Baraza
la Vijana Zanzibar Salum Issa Ameir, amesema vijana waliojiunga na mabaraza ya
vijana katika Wilaya zote za Pemba ni 9,308 wanaume wakiwa 4,754 na wanawake ni
4,553 sawa na asilimia 48% ya vijana wakike waliojiunga na mabaraza hayo,
ambapo Wilaya ya Micheweni Vijana wa kiume waliojiunga baraza la vijana ni
1,078 na wanawake wakiwa 952, Wilaya ya Wete wanaume 1,176 wanawake 1,041,
Wilaya ya Chake Chake wanaume 1,260 wanawake 1,386 na Wilaya ya Mkoani wanaume
1,240 wanawake 1,174. Idadi inayojumuisha Vijana wakiume 4,754 na wanawake
4,553 sawa na asilimia 48% ya vijana wote waliojiunga na mabaraza hayo Kisiwani
Pemba.
“Uendeshwaji sio rafiki”
Ali Omar Juma miaka 28,
mkaazi wa Wawi Chake Chake amesema malengo ya uanzishwaji wa mabaraza ya vijana
ni mazuri lakini mifumo ya uendeshaji wa mabaraza hayo sio rafiki kuanzia njia
ya upatikanaji wa wanachama na namna yanavyoendeshwa huku akijitolea mfano yeye
mwenyewe kushindwa kujiunga na baraza la vijana Wilaya ya Chake Chake kutokana
na dana dana aliyokumbana nayo alipotaka kujiunga kwa kile tu anachofikiri kuwa
ni mfuasi wa chama fulani cha upinzani.”Nilitamani
kujiunga na baraza la vijana lakini nimeshindwa kutokana na uendeshwaji wake,
ukisoma Sera na malengo ya uanzishwa wa mabaraza ya Vijana ni mzuri sana lakini
malengo hayo yanashindwa kufikiwa kutokana na uendeshwaji wa mabaraza hayo”
Ameendelea kusema kuwa hata upatikanaji wa wanachama unaangalia zaidi chama
Fulani “Mfumo hautowi nafasi kwa kila kijana anaejisikia kuwa mwanachama
ajiunge ,maana ukiangalia asilimia kubwa ya vijana waliomo kwenye mabaraza hayo ni
vijana wa chama tawala” Amemaliza Ali.
Hali hii inaungwa mkono na
Hafsa Maulid Azizi 22, Mkaazi wa Shehia ya Wesha Wilaya ya Chake Chake Pemba ambaye pia ni
mwanafunzi wa fani ya Biashara ngazi ya Astashahada Chuo cha Samail kilichopo
Gombani, amesema anasikia tu kuhusu kuwepo
mabaraza ya vijana lakini hana taarifa za kutosha kuhusu mabaraza hayo.“Toka nipo Sekondari na sasa nipo chuo
sijawahi kupata taarifa wala elimu yoyote kuhusu mabaraza ya Vijana sifahamu
wapi zipo ofisi zake wala vipi naweza kujiunga sasa hapo kweli tutasema
mabaraza ya vijana yapo kwa vijana wote kwa kwa baadhi tu?” Amehoji Hafsa huku akiwataka viongozi wa Mabaraza ya Vijana
kutafakari upya mwenendo wa Mabaraza hayo ili yaweze kufanya kazi kwa uadilifu
katika kuwafikiwa vijana.
“Lengo la Kuundwa”
Baraza la Vijana Zanzibar limeundwa kwa mujibu wa matakwa ya Kisera na Kisheria yanayoelekeza haja ya kuwajenga vijana kuutambua utaifa wao, hali ya umoja na mshikamano na kujiheshimu, pia kufanya kazi kama ni jukwaa na kiungo wakilishi kwa masuala ya vijana Zanzibar, kushajihisha kujengewa uwezo vijana ili kuwafanya wazalishaji katika jamii na kuwakilisha maslahi ya vijana ndani na nje ya nchi.
Baraza la Vijana ni Chombo
kinachojitegemea kilichoanzishwa chini ya Sheria namba 16 ya mwaka 2013 ambayo
imetiwa Saini tarehe 30/06/2014 na aliyekuwa Rias wa awamu ya saba wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Ali Mohamed Shein.
Kisiwa cha Pemba kina jumla ya Wilaya nne ambazo ni Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni na Wilaya zote hizo zina mabaraza ya vijana ambayo huwalea vijana na kuwafinyanga kuwa viongozi bora wenye nidhamu, maadili, uzalendo pamoja na kuwa na uthubutu wa kiutendaji katika nafasi mbali mbali
“Isemavyo Sera”
Ibara ya 6 ya Sera ya
uanzishwaji wa Mabaraza ya Vijana inaeleza usawa wa kijinsia katika mabaraza
hayo kwa mujibu wa mgawanyo wa nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya Shehia,
Wilaya hadi Taifa, mfano katika usawa huo wa kijinsia ni pale kifungu cha 2
katika ibara hiyo 6 kueleza kuwa kutakuwa na Mwenyekiti na Makamo Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana katika ngazi ya Wilaya kwa kuzingatiwa utofauti wa kijinsia.
“Baraza limenipatia nafasi”
Saumu Mohammed Said 31,
mkaazi wa Majanzi Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambaye kitaalum
ni mwalimu taaluma .Mwaka 2020 Saumu ameteuliwa kuwa Diwani wa Wadi ya Wingwi Micheweni
kabla ya uteuzi huo anashikilia nafasi ya Mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana Taifa katika Wilaya ya Micheweni, Mjumbe
wa Baraza Kuu Mkoa wa Kaskazini Pemba UVCCM mwaka 2017 hadi 2022, Mwenyekiti wa
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wadi ya Sizini pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati
ya Propaganda na Uenzi Wilaya ya Micheweni kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Amesema “Kwa asilimia 90% naweza kusema mchango wa
baraza la vijana ndio umeniwezesha kuteuliwa kuwa diwani kwasababu kama
nisingekuwa kwenye baraza la vijana nisikuwa na uwezo au kuonekana kuwa naweza
kushika nafasi hiyo na nikaweza kuifanyia kazi ipaswavyo” Amesema Saumu.
Licha ya kuwa kwenye Baraza la Vijana lakini Saumu amesema “Vijana wakike tunakabiliwa na changamoto nyingi zinazowakabili kwenye Baraza ikiwemo uhaba wa Wanawake wanaojiunga na Mabaraza kutakiwa kimapenzi na baadhi ya viongozi wa Mabaraza hayo, Rushwa ya ngono pamoja kukatishwa tamaa ya kutokutimiza ndoto zao” Amemaliza Saumu.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chake Chake Zulekha Maulid Kheri 28, amesema Mabaraza ya Vijana yana mchango mkubwa katika kuwaandaa Wanawake kuwa viongozi imara kwani huandaa mafunzo maalumu ya Uongozi kwa Vijana mafunzo huwawezesha vijana hao kujitambua na kukaa katika mstari nyoofu wa kushika nafasi za uongozi
"Nilijunga na Baraza la Vijana Chake Chake tangu nikiwa na umri wa miaka 19 hadi sasa nina umri wa miaka 28 naona faida ya kuwa mwanachama wa Baraza la Vijana kwani hata hii nafasi ya Makamo wa Baraza la Vijana ninayoshikilia kwasasa imetokana maandalizi mazuri nikiwa ndani ya Mabaraza"
Ruwaida Mohammed Omar 30, ni Makamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Mkoani, amesema Mabaraza ya Vijana yana mchango mkubwa katika kuwaandaa wanawake kushika nafasi za uongozi kwa kwa kuwepo usawa wa kijinsia pamoja mafunzo mbali mbali ya uongozi.
“Mabaraza
ya Vijana yana mchango mkubwa sana katika kuwaandaa Vijana wakike kushika
nafasi za Uongozi kwasababu unapokuwa mwanachama au kiongozi wa Baraza kuna
mafunzo ambayo yanaandaliwa kwa ajili ya Vijana ambayo yanakupa mwelekeo wa
namna ya kuwa Kiongozi bora” ameendelea kusema kuwa “Mimi hadi sasa
nimeshashika nafasi za Uongozi zaidi ya nne kutokana na uzoefu niliopata katika
Baraza la Vijana” Amemaliza Ruwaida.
Wakuu wa Wilaya ni walezi
na wasimamizi wa Mabaraza ya Vijana kwa
ngazi ya Wilaya, Mgeni Khatib Yahya ni Mkuu wa Wilaya ya Micheweni na Mlezi wa
Baraza la Vijana la Wilaya hiyo amesema katika kuhakikisha wasichana na
wanawake wanapatiwa fursa ya kujiunga na Baraza la Vijana ameweka utaratibu wa
kukutana na Vijana wakike wa Wilaya hiyo kila mwaka “Nikiwa mlezi wa Baraza la
Vijana Micheweni nahakikisha wasichana na wanawake hasa wale wanaosoma kuanzia
Sekondari na Vyuoni tunawapa elimu na kuwaonesha faida za kujiunga na Baraza la
Vijana na tunashukuru kuona muitikio unaridhisha”. Amesema.
Akizungumzia juu ya kuwepo
kwa Malalamiko ubaguzi wa kichama kwenye mabaraza hayo Mkuu huyo wa Wilaya ya
Micheweni amesema “Ni kweli hayo malalamiko
yapo tangu mimi sijateuliwa kushika nafasi hii tangu mimi mwenyewe niko kwenye
hayo Mabaraza lakini ukweli ni kwamba sio kwamba Vijana wa CCM ndio walengwa
haya Mabaraza yameanzishwa kwa ajili ya Vijana wote wenye sifa sema tu Vijana
wengi wenye muamko wa kujiunga na Mabaraza ni Vijana wa CCM” Amemalizia Mgeni.
“Tunawapata kwa kuwapa
Elimu”
Abdalla Saleh Issa ni
Mwenyekiti wa baraza la Vijana Wilaya ya Mkoani Pemba amesema njia ambazo
wanazitumia kutoa taarifa na elimu kwa vijana ili kujiunga na mabaraza ya
vijana ni pamoja na mabonanza, mikusanyiko ya vijana, vikundi vya
wajasiriamali, mikutano ya kijamii, siku ya mwenge wa uhuru, vipindi vya radio
pamoja kutoa vipeperushi.“Sio
kweli kwamba vijana wengi hawana elimu ya Mabaraza ya Vijana kwasababu viongozi
wa Mabaraza Vijana tunatumia njia mbali mbali kutoa kuhusu mabaraza ya Vijana na
wengi tunawafikia mijini na Vijijini” Amesema Abdallah.
“Elimu na muamko uwepo“
Katika kuhakikisha usawa
wa kijinsia unafikiwa katika vyombo vya kutunga Sheria na hata nafasi mbalimbali
za Uteuzi Serikalini, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA –
Z,Fat-hia Mussa Said ni Mratibu wa Tamwa, Pemba amesema “Tamwa Zanzibar tunaendelea programu mbali mbali zenye lengo la
kuhakikisha tunaongeza idadi ya viongozi wanawake katika vyombo vya maamuzi
kama vile Baraza la Wawakilishi na Bunge.” Akiongezea suala la usawa kwenye
ngazi za uongozi Fat-hiya ameongeza kuwa “Vyombo vya maamuzi tu vinaanza ngazi
ya usheha na udiwani nafasi za uteuzi za Serikali kwa mfano kwasasa tuna Katibu
Mkuu Kiongozi wa kwanza Mwanamke Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa kwanza mwanamke Pemba
Mheshimiwa Salama yote hayo ni miongoni mwa matunda ya programu zetu”
Comments
Post a Comment