“SMILE PEMBA MARATHON” KUBORESHA USTAWI WA WATU WENYE ULEMAVU
Na, Hassan Msellem- Pemba
Wananchi Kisiwani Pemba wametakiwa kushiriki mashindano ya Mbio yanayobeba jina la Smile Pemba Marathon ili kufanikisha lengo la Mbio hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Ahmed Abuubakar Mohammed huko Gombani Pemba, amesema lengp la Mbio hizo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba na vifaa saidizi kwa watu Wenye Ulemavu.
Aidha amesema Mbio hizo za hisani zinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2024, katika Uwanja wa Gombani Pemba kwa kukusanya wanariadha kutoka ndani na nje ya Nchi, ambapo Mgeni rasmi wa mbio hizo anatarajiwa kuwa makamo wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla
“Naomba nitowe wito wangu kwa wananchi Watanzania wote wapenda maendeleo kuweza kushiriki katika mbio hizi na pia kuweza kutoa michango yao kwa ajili ya kusaidia Watu Wenye Ulemavu” amesema
Aliongeza kuwa Mbio hizo zinatarajiwa
kuwa mbio za Nusu Marothon zikijumuisha mbio za Kilometa 21, Kilometa 10 na Kilometa
5 sambamba na mbio za Baiskeli ya magurudumu matatu (Tricycle Racing) ambazo zinatarajiwa
kuanza saa 12:30 Asubuhi
Kwa upande wake Meneja Mkaazi Pemba wa Kampuni ya TTCL Khamis Is-haka Ngwali, amesema wamemua kuwa wadau wa Mbio hizo kwa lengo na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha hali za watu wenye ulemavu zinaimarika
Amesema “Licha ya kufanya biashara tumeguswa na programu hii ya wenzetu wa SMILE ya kuwasaidia ndugu zetu wenye mahitaji maalum programu hii ya kuchangisha vifaa itawasaidia ndugu zetu hawa wenye uhitaji maalum kupata vifaa au nyezo kwa mfano ukimsaidia kigari mtu mwenye Ulemavu umemsadia nyezo ya kusafiri na kufanya shughuli zake za kimaendeleo na kujenga Uchumi wetu kwahivyo kama taasisi ya Umma tumeshiriki katika hili zoezi kuwajengea uwezo wenzetu hawa wenye ulemavu wapate vifaa ili waweze kufanya shughuli zao za kimaisha ikiwa ni sehemu ya kuiunga mkono Serekali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar”
Arif Mohammed Said, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Pemba, amesema kwa dhati wamekubali kuunga juhudi za Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais kwa kuchangia vifaa tiba na vifaa wezeshi kwa watu wenye Ulemavu Ili kuweza kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu ambao ni sehemu ya walipa Kodi.
Sambamba na hayo Meneja huyo amewataka Wananchi kuachana na dhana kwamba Kodi zinazokusanywa Zanzibar haziwanufaishi Wazanzibari na badala yake kufahamu kuwa taasisi zote za Kodi za TRA na ZRA zinafanya kazi ya makusanyo kwa mujibu wa Sheria na kwamba Kodi hizo zinatumika kwa maslahi ya Wananchi wote wa Bara na Visiwani.
Gharama za usajili wa Mbio hizo ni shilingi elfu thelathini za Kitanzania kwa kila mshiriki na kwa upande wa wawashiriki wan je Tanzania ni Dola 10, ambapo gharama za malipo zitafanyika kwa njia ya simu kupitia kwenye nambari 15115602 Tigipesa yenye jina la Smile Pemba Marathon
Mbio za Kilometa 21 zitaanzia Gombani Kongwe, kupitia Mjini Chake Chake, Afrikana, Kichungwani, Qatar, Tibirinzi, Pondeani, Pagali na Kumalizia Gombani Mpya, Mbio za Kilometa 10 zitaanzia Gombani Kongwe kutipia Machomane, Msingini, Tume huru ya Uchaguzi, Sukita, Banki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Machomane na kumalizia Gombani Mpya.
Kilometa 5 Mbio zitaanzia Gombani Kongwe, kupitia Machomane, Msingini, Tume huru ya Uchaguzi, Sukita, Banki, Machomane na kumalizia Gombani Mpya, na kwa upande wa Mita 100 ambazo ni kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu zitafanyika ndani ya Uwanja wa Gombani.
Wadau wa Kuu wa Mbio hizo ni Kampuni ya simu ya TTCL, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA)
Zawadi za washindi wa Mbio hizo zitatangazwa mara tu utaratibu wa ugawaji wa zawadi hizo utakapo kamilika.
Kwa
mawasiliano zaidi kuhusu Mbio hizo unaweza kupiga simu nambari
+255773538539 au +255777671211 au +255773818117
Comments
Post a Comment