NA, HASSAN MSELLEM, PEMBA
Katika jamii nyingi kumekuwa na tamaduni ambazo zimekuwa zikiwanyima fursa watu wenye ulemavu wakiwemo wanawake katika kushiriki kwenye michezo kwa kile wanachodhani kuwa watu hao kuwa hawana uwezo wa kushiriki michezo.
Pamoja na juhudi zinazochukuliwa Serikali na wadau mbali mbali katika kuondosha changamoto hiyo lakini bado wapo baadhi ya wanajamii na uwazi wa uthubutu katika kuwapambania watu hao kwenye mambo ya msingi ikiwemo elimu na hata kushiriki katika michezo.
Rashid Hamad Khamis, ni Katibu wa timu ya watu wenye Ulemavu Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema jamii haijatilia mkazo kwa watu wenye ulemavu wa akili katika kushiriki michezo hali inayosababisha kundi hilo kuachwa solemba kwenye michezo.
"Miongoni mwa madai ya wazazi juu ya kutowaruhusu kuingia kwenye michezo ni pamoja na kutokuwaamini juu ya mazingira yao kutokana na ulemavu wao jambo linawanyima haki hiyo ya kushiriki kwenye michezo" alisema katibu huyo
Akizungumza juu ya namna ya walivyo jiandaa alisema kuwa hivi sasa wameandaa utaratibu maalumu wa kuwapitia wazazi kuwaelimisha wazazi wa watoto wenye ulemavu ili kuwapa uelewa juu ya watoto hao kushiriki kwenye michezo
"Tunajaribu kuwafahamisha Wazazi wa watoto wenye ulemavu kuwa kuwanyima fursa ya kushiriki michezo watoto hao ndani ya jamii bado ni tatizo kubwa ambapo bila ya kutambua kuwa ni kuwanyima haki zao pamoja na kuwanyanyapaa" alisema.
Hata hivyo alisema ingawa kwa sasa wameweza kuanzisha timu moja tu ya watu wenye ulemavu kwa wanaume lakini kutokana na umuhimu huo wataanzisha timu maalumu ya Wanawake
"Katika msimu ujao tumeandaa mashindano ya watu wenye ulemavu kwa timu mbili za wanawake na wanaume ili kwa lengo la kutoa haki sawa ya michezo kwani kufanya hivyo kutayaweka karibu na jamii makundi hayo ambayo yamesahaulika" aliongeza
Mratibu wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk, ameeleza kuwa wamekuwa wakielimisha jamii juu ya namna ya kuishi na watu hao kwa kuwashirikisha katika mambo mbali mbali ikiwemo kushiriki katika michezo.
Alisema baraza lina jukumu la kuwasajili na kuwatambua pamoja na kuwasaidia kwa vitu mbali kupitia watu ambao wamekuwa wakiwatafuta kuyaangalia makundi hayo.
"Sisi Baraza la Watu wenye ulemavu tumekuwa na jumuku la kuwasajili kuwatambumbua ili lengo letu nikuona watu hao wanasaidiwa,tumekuwa tukitafuta watoto wa aina hiyo" alisema.
Alinena mara nyingi makundi ya watu hao yamekuwa yakiwekwa nyuma na kukoseshwa haki zao za msingi lakini baraza limekuwa likiwakutanisha na watu tofauti kutoa elimu ya kutokulibagua kundi hilo
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar,ya Mwaka 1984 kifungu 12 (1) kina fafanua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa.
Shekh Naasor Abdalla Mauli ni Mwanaharakati wa mambo mbali mbali ya kijamii yakiwemo ya usawa wa kijinsia amesema Dini ya Kiislamu imehimiza suala la usawa kwani wanadamu wote ni sawa licha ya tofauti zao za kimaumbile
Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania Zanzibar,Ofisi ya Pemba Fthiya Mussa Said, aliongeza kuwa Tamwa imekuwa ikitunana na wadau mbali mbali katika kushajihisha wanawake kupewa fursa na kama wanaume katika kushiriki michezo.
Alisema ukiangalia duniani wanawake wengi wamekuwa wakionekana kwenye mashindano tofauti hali hiyo inaonesha wanawake wanaweza lakini kwa upande wa Pemba,bado jamii inawanyima nafasi wanawake kushiriki michezo.
Waziri Tabia anasema, kwa upande wa michezo ya watu wenye ulemavu wa mguu mmoja na mkono mmoja, Wizara imefanikiwa kulisaidia Shirikisho la mchezo huo, kushiriki mashindano ya Kitaifa yaliyofanyika Arusha.
Lakini hata Shirikisho la michezo ya Viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA) limesaidiwa kuandaa bonanza, kwa ajili ya shamra shamra ya kuadhimisha siku ya viziwi duniani.
Sheria ya watu wenye ulemavu namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (9) kimesema watu wenye ulemavu wanayo haki ya kushiriki kwenye michezo na burudani.
TAMKO LA SERA YA MICHEZO YA MWAKA 2018
Serikali itahakikisha Watu Wenye Ulemavu wanawekewa mazingira yanayofaa, kuwawezesha kupata fursa sawa na haki ya kushiriki mashindano mbali mbali kwa uwezo wa hali zao.
MWISHO.

Comments
Post a Comment