"UCHUMI WA BULUU NI BIASHARA KATI YA SERIKALI NA BENKI YA CRDB CRDB" MWENYEKITI WA ADC TAIFA-SHABANI ITUTU.
Na, Hassan Msellem, Pemba
Mwenyekiti wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Taifa Shabani Itutu, ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu kuboresha hali za Wananchi kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu, ambayo mpaka sasa haijafikiwa ipaswavyo.
Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wanachama wa wa Chama cha ADC na Wananchi mbali mbali Kisiwani Pemba, amesema licha ya Serikali ya awamu ya nane kuanzisha Sera ya Uchumi wa Buluu kwa lengo la Kuboresha Hali za Wananchi kupitia rasilimali za baharini ikiwemo uvuvi wa Samaki na zao la mwani bado hali za Wananchi kupitia rasilimali hizo hazijaimarika.
Akitaja sababu zinazobabisha kutokufikiwa kwa Sera ya Uchumi wa buluu kwa Wananchi ni pamoja kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya uvuvi, kukosekana kwa viwanda vya kusindika samaki pamoja kutokufanya kazi kwa viwanda vya kuchakata zao la mwani.
"Tunaamini dhamira ya Serikali ni njema sana kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu lakini dhamira hiyo haiwezi kufikiwa endapo Serikali itashindwa kununua meli za kisasa zinazoweza kwenda kwenye kina kirefu cha maji, kuwa na uwezo mzuri wa kuhifadhia tani za kutosha za kuhifadhia samaki pamoja kuwa na viwanda vya kusindika samaki, pamoja kufanya kazi kwa viwanda vya kuchakata mwani ambavyo vimezinduliwa hivi karibuni" alisema
Akifanya ziara katika kaburi la aliyekuwa Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Marehemu Mwalim Seif Sharif huko Mtambwe Nyali, amewataka wanasiasa na watendaji wa Serikali kufuata nyayo za Kiongozi huyo Ili kuwaletea Wananchi Maendeleo bila ya ubaguzi.
"Naomba niwasihi sana viongozi vyama mbali mbali vya siasa pamoja watendaji wa Serikali kuenzi na kufata nyayo za marehemu Maalim Seif Sharif Hamad katika kuwatumikia Wananchi, Marehemu hakuwa na misingi ya ubaguzi Wala dhulma katika kipindi Chake chote cha kuwatumikia Wananchi na ndio maana leo tunamuenzi kwa heshima kubwa"
Kwa upande wake Katibu wa chama cha ADC Taifa Mwalimu Hamad Azizi, amesema chama cha ADC ni miongoni mwa vyama 19 Tanzania vilivyopatiwa Usajili kikiwa na miaka 13 tangu kuanzishwa kwake, hivyo basi amewataka Vijana na Wananchi kujiunga na Chama hicho Ili kunufaika na Sera, Ilani, malengo yanayotokana na Chama hicho.
Akitoa ufafanuzi kuhusu ubovu wa barabara ya Mtambwe Nyali Hadi Uondwe, amesema tayari Uongozi wa Chama hicho umeshazungumza na Serikali Ili kuhakikisha tatizo la ubovu wa barabara hiyo linatatuliwa.
Nao baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa TAWI la Chama hicho huko Mtambwe, wamesema wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara hali inayowasababisha kushindwa kufanya shughuli zao zakimaisha ipaswavyo.
"Kwakweli changamoto yetu kubwa ni ubovu wa barabara tunapata shida sana sio kwa kipindi hichi cha jua wala mvua kwasababu Barabara ni mbovu sana hata hivyo vinavyokuja huku vinaharibika Kwahivyo inatubidi tutembee kwa miguu kwenda kwenye shughuli zetu mbali mbali" alisema mmoja wa Wananchi hao
Katika Ziara hiyo ya ufunguzi wa matawi mwenyekiti wa ADC Taifa Ndugu Shabani Itutu alifungua TAWI la Chama cha ADC Kinazini, na Nyali huko Mtambwe, Tawi la ADC Jombwe na Chole Kengeja, na kuwakabidhi kadi za uanachama kwa viongozi na wanachama wa matawi hayo pamoja na kutembelea kaburi la aliyekuwa Waziri Kiongozi Dr. Omar Ali Juma Mgogoni na aliyekuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko Mtambwe Nyali.
Comments
Post a Comment