BONANZA LA MICHEZO KUIBUA VIPAJI VYA WANAMICHEZO WANAWAKE PEMBA.

Na, Hassan Msellem, Pemba.


CLUB ya mazoezi ya viungo Gombani fitness kwa kushirikiana na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar pamoja na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) wameandaa bonanza la michezo na mazoezi Kisiwani Pemba litakaloanza shamra shamra zake kuanzia kesho tarehe 20 na kufikia kilele siku ya tarehe 28.07.2024 huu kwa kufanyika matembezi ambapo zaidi ya washiriki 500 kutoka nje ya kisiwa cha Pemba wanatarajiwa kushiriki katika bonanza hilo.


Akizungumza Mratibu wa Bonanza hilo KHalfan Amour Muhamed ambae pia ni Katibu wa Gombani fitness, alisema kuwa lengo Bonanza hilo litakaloanza na matembezi kutoka Madungu hadi uwanja wa Gombani kuanzia saa 12 za asubuhi ni kusaidia kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana kwa kushirikisha na kukuza usawa wa kijinsia katika michezo ya aina mbali mbali kwa wanawake kisiwani humo .


Amesema Club hiyo kwa kutambua juhudi zinazofanywa na wadau wa michezo kwa wanawake wameona kuna umuhimu mkubwa wa kulitumia bonanza hilo la miaka kumi kuunga mkono na kuhamasisha kukuza usawa wa kijinsia katika michezo kwa kuwashirikisha viongozi mbali mbali wa serikali taasisi binafsi pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti.


Aidha mratibu huyo amesema kuwa jumla ya michezo mitatu inatarajiwa kuchezwa katika siku ya kilele cha maadhimisho hayo ambayo ni pamoja na mchezo wa mbio za magunia ,mchezo wa kuvuta kamba pamoja na mchezo wa mazoezi ya viungo ambayo itashirikisha jinsia zote katika kuonesha vipaji vyao walivyo navyo.


Akizungumzia kuhusu shamra shamra zitakazoanza kesho mratibu huyo amesema kuwa waandaaji wa bonanza hilo wamedhamiria kupita katika maeneo mbali mbali kutoa elimu kwa jamii, na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika mazoezi na michezo,sambamba na kutoa elimu juu ya kujikinga na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi na wasichana kupitia mbinu mbali mbali za michezo.


Kwa upande wake mratibu wa Tamwa Pemba Fat-hiya Mussa Said, alisema kuwa lengo la chama hicho kuunga mkono juhudi za club hiyo katika maadhimisho ya kutimiza miaka 10 ni kusaidia kuongeza uelewa kwa jamii juu ya umuhimu wa michezo kwa maendeleo.


Aidha amewataka wananchi maeneo mbali mbali kujitokeza kushiriki na kuangalia k michezo ya vol ball,basket ball pamoja na mpira wa miguu itakayozikutanisha timu mbali mbali za wanawake pamoja na wanafunzi itachezwa katika viwanja tofauti kufuatia shamra shamra za bonanza hilo .


Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa shirika la Bima Zanzibar ofisi ya Pemba Khatib Bakar, alisema lengo la Bima ni kumrejesha mtu katika hali yake hivyo, aliwashauri wanamichezo kukata bima ambazo zitawarejesha pale ambapo walikua kabla ya kupata majanga.


Kupitia Bonanza hilo ambalo limebeba kauli mbiu ya "WEKEZA KATIKA MAZOEZI NA MICHEZO KWA JINSIA ZOTE" huduma za kujiunga na bima za majanga mbali mbali pamoja na elimu juu ya bima zinazotolewa na ZIC zitatolewa.



Comments

Popular posts from this blog

MWALIMU WA MADRASA MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE

Mama ajifungua kisha kukiua kichanga na kukifukia kwenye tuta- Sizini Pemba

Mtangazaji wa Wasafi Media, Dida Afariki Dunia