Weledi, umahiri katika kada ya habari ni nguzo muhimu.
Waandishi wa habari wametakiwa kufuata kwa kina maadili ya waandishi wa habari ili kukuza weledi na umahiri wa kada ya habari na kuzifanya taasisi za kihabari ziweze kuaminika na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Akizungumza na wadau wa habari katika ziara yake iliyofanyika Zanzibar tarehe 23 na 24 Machi katibu mtendaji wa baraza la habari Tanzania Ernest Sungura amesema kuwa katika kufuata maadili hayo pia suala la kuzingatia vyanzo anuai vya habari havina budi kupewa kipaumbele.
“Mara nyingi waandishi wetu wamekuwa na maradhi ya chanzo kimoja cha habari hali hii inapaswa kubadilika ili habari zetu ziweze kuwa na mawanda mapana zaidi na vyanzo vingi na tofauti vya habari”, alisisitiza.
Amesema kuwa nguvu ya vyombo vya habari haina budi kutumika katika kujenga jamii iliyo bora na hivyo sauti za watu hazina budi kupewa kipaumbele.
“taasisi za habari na vyombo vya habari havina budi kubadilika ili sauti za makundi ya pembezoni ikiwemo wanawake na vijana ziweze kusikika tuwape sauti wale wasio na sauti”,
aliongeza.Akizungumzia kuhusu masuala ya jinsia katika vyombo vya habari amesema kuwa bado waandishi wa habari wanawake hawakupewa fursa zinazostahiki na hivyo kunatakiwa juhudi zaidi katika kuimarisha waandishi hao.
Wahariri wana dhima na dhamana ya kuwanyanyua waandishi wanawake ili wawe mahiri katika kazi zao lakini na wamiliki na viongozi wawape nafasi ya kuwemo katika nafasi mbali mbali za uhariri ili usawa na haki kwa jinsia zote uweze kupatikana.
"Baraza la habari linathamini mchango wa wanawake katika kuimarisha kada ya habari na baraza lina mradi maalum ya kuimarisha haki na usawa wa jinisia katika vyombo vya habari" alifafanua
Hata hivyo alikiri kuwa utafiti wa baraza la habari Tanzania wa mwaka 2019 umebainisha kuwa ingawa wanawake wapo katika vyombo vya habari lakini bado nafasi za ngazi za juu ikiwemo wahariri bado zimedhibitiwa na wanaume.
“HIvyo basi ili kuimarisha hayo katika mradi maalum wa baraza la habari wa kuwanyanayua wanawake katika vyombo vya habari unaofadhiliwa na shirika la Vikes la serikali ya finland kuna mkakati maalum wa kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi kwa wanawake katika vyombo vya habari “, alifafanua.
Alivitaka taasisi za kihabari kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha kada ya habari pamoja na kuwafanya waandishi wa habari wafanye kazi zao kwa weledi na umahiri.Mkurugenzi wa tamwa Zanzibar Dk. Mzuri issa amesema kuwa Tamwa itaendelea kufanya kazi kwa karibu na MCT katika suala zima la kuimarisha kada ya habari lakini pia kukuza na kuimarisha weledi wa waandishi wa habari wanawake.
“Tuna umoja wa taasisi za habari unaojulikana ZAMECO chini ya umoja huu tunafanya kazi za kuimarisha kada ya habari ikiwemo kufanya uchechemuzi wa shaeria za habari za Zanzibar “ alifafanua.
Mhariri mtendaji wa shirika la magazeti ya serikali Ali Mwadini amesema kuwa weledi na umahiri ni muhimu katika kada ya habari na kuimarisha kwa kina vyumba vya habari ili kuwe na madawati maalum ya kushughulikia habari tofauti.
“Kunahitajika madawati ya habari za uchunguzi, habari za vijijini ili kuvifanya vyombo vyetu viweze kuandika habari ambazo zitaibua kero za wananchi na hususan wa vijijini”, aliongeza.
Vyombo vyetu vya habari vimetawaliwa na habari za mjini na habari za matukio hali hiyo inatakiwa ibadilike ili viweze kuleta mabadiliko katika jamii.
Katibu wa Zanzibar Press Club Mwinyimvua Nzukwi alisema kuwa kufanya kazi kwa pamoja ni nguzo muhimu ya kuimarisha kada ya habari na hivyo Zannzibar Press Club itaendelea kushirikiana na Baraza la habari ili kuleta maendeleo katika kada ya habari.
Katibu mtendaji wa baraza la habari Tanzania Ernest Sungura amefanya ziara rasmi ya siku mbili hapa Zanzibar ikiwa ni shemu muhimu ya kukuza na kuimarisha mahusiano kwa taasisi za habari pamoja na kuimarisha kazi za baraza la habari hapa nchini.
Katibu mtendaji alitembelea ofisi ya watetezi wa haki za binaadamu ofisi ya zanzibar, Tamwa Zanzibar, Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar, na shirika la magazeti ya serikali. End.
Comments
Post a Comment