HASSAN MSELLEM - PEMBA Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inaungana na wanaharakati, wanahabari, na watetezi wa haki za binadamu duniani kote, kuadhimisha siku ya Haki za Binaadamu ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 10 Disemba ya kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu, haki za binadamu kama “Mahitaji ya Kila Siku”, inasisitiza kuwa haki hizi lazima zilindwe bila kusuasua kila siku, kwa kila mtu, na katika kila mazingira. Katika maadhimisho ya mwaka 2025, ZAMECO inasisitiza kwamba uhuru wa kupata na kutoa taarifa ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa kulinda haki nyingine zote za binadamu. Haki hii haipaswi kutazamwa kama ridhaa ya mamlaka bali kama wajibu wa kikatiba na kimataifa unaopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa. Tunawakumbusha wadau wote kuwa tangu kupitishwa kwa Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR) mwaka 1948 uhuru wa kujieleza umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha kwamba jamii inakuwa na nguvu ya kushiriki, ku...