Skip to main content

Waandishi wapigwa msasa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (ECD)

 NA, HASSAN MSELLEM-PEMBA

Waandishi wa habari Zanzibar wametakiwa kuripoti na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na taifa lenye ustawi bora.

Akizungumza na waandishi na wadau hao katika mafunzo ya siku nne yaliyofanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya Jamirex Mwenge Jijini Dar- Es- Salaam Katibu Mkuu kutoka Wizara ya elimu Zanzibar Dkt. Khamis Abdalla, amesema Dira ya maenedeleo endelevu ya 2050 ya Zanzibar itafikiwa endapo watoto watakuwa katika makuzi na malezi bora yenye kujenga maadili na maarifa

Aidha, Dkt. Khamis amewataka waandishi hao kuandaa vipinda, ripoti na Makala mbali mbali zitakazochochea haki za Watoto ikiwemo haki kupata elimu, chanjo, vyeti vya kuzaliwa na kuwalinda na kuwahifadhi.

Kwa upande wake Meneja mradi Bi. Mariam Issa,  amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imeamuaa kuongeza nguvu katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kutokana na umuhimu wa rika hilo katika makuzi bora ya afya ya mwili na akili ya mtoto.

“kwahivyo licha ya Serikali kupitia Wizara ya afya kuboresha huduma za afya imeona kuna haja kubwa ya kuongeza nguvu katika makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia umri mwaka 0 hadi miaka 8 ili kuwa na Watoto wenye afya bora ya kimwili na kiakili” Alisema

Meneja Mradi Bi. Mariam issa

Mapema akizungumza katika mafunzo hayo mtaalamu wa malezi, makazi na maendeleo ya awali ya mtoto kutoka taasisi ya Children in Grassfire Davis Gisuka, amesema malezi na makuzi ya mtoto yanaanza tangu mtoto akiwa tumboni kwa mama hadi kufikia umri wa miaka nane ikiwemo kuwasiliana, lishe na kujifunza.

Alisema “makuzi ya mtoto huanzia tangu akiwa tumboni kwa mama yake na ndio maana tunasema kuanzia 0 hadi miaka 8, hivyo wazazi wanatakiwa kuwasiliana vizuri na mtoto, mama anapaswa kula vyakula vyenye lishe kuwasiliana nae vizuri ili kuimarisha afya ya mtoto kimwili, kiakili na kitabia”

Mtaalamu wa malezi, makazi na maendeleo ya awali ya mtoto kutoka taasisi ya Children Grassfire bwana Devis Gisuka

Naye, Muwezeshaji kutoka Madrasa Childhood Bi. Sharifa Suleiman Majid ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia mfumo bora wa makuzi ya mtoto ni pamoja na kuwa na afya bora, lishe, elimu ya mapema, malezi yenye uwajibikaji, ulinzi na usalama wa mtoto.

“Shirika la afya Duniani (WHO) UNICEF, Benki ya Dunia NCF wameainisha mambo Matano muhimu yanayohusu makuzi bora ya mtoto ambayo ni lishe, elimu ya mapema, malezi yenye uwajibikaji pamoja na ulinzi na usalama nav yote hivyo hakuna bora zaidi kuliko vyengine vinategemeana kwahivyo munapaswa kuelimisha jamii juu ya mambo hayo ili waweze kufahamu umuhimu wake” Bi. Sharifa Suleiman

Muwezeshaji kutoka Madrasa Childhood Bi. Sharifa Suleiman Majid.

Nao, baadhi ya wanahabari hao wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa kuelimisha jamii pamoja kuripoti taarifa za matukio mbali mbali yanayohusu Watoto ili kuhakikisha jamii inapokea mabadiliko chanya kuhusu makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto

“Kwa hakika mafunzo haya yametupa mwanga wakutosha kuhusu mambo ya ECD ni jukumu letu sasa waandishi kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii pamoja kuandika na kuripiti taarifa mbali mbali ya makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto ili jamii zetu ziweze kupata mabadiliko chanja juu ya mausla haya na kwa niaba ya waandishi wenzangu tunaahidi kuyafanyia kazi ipaswavyo mafunzo haya” Mwinyimvua Nzukwi Katibu Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) 

Mafunzo hayo kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa waandishi wa Habari na wadau wa afya Zanzibar yameandaliwa na Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini Zanzibar (ZPDB) kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali ikiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania na kunafadhiliwa na UNICEF

Comments