“Nimeshiriki michezo tangu nikiwa darasa la tatu kwasasa ni kocha wa timu ya wanawake ya mpira wa miguu maadili yangu ya Kizanzibari yako pale pale” Tamasha Kocha wa timu-Wete Women Club
Makala Na, Hassan Msellem-Pemba
Mpira wa Miguu au wengi wanapenda kuita Soka, Kandanda, Ndinga au Kabumbu yote yakiwa ni majina sahihi kwa mujibu wa wapenzi wa mchezo huo. Unachezwa uwanjani ukiwa na jumla ya wachezaji 22 kila timu ikiwa na wachezi 11, lengo la mchezo huu ni wachezaji kumiliki mpira kwa kutumia miguu kwa shebaha ya kufunga goli yani kuingiza mpira kwenye wavu zilizosimamishwa kwenye milingoti mitatu yani kulia, kushoto na juu.
Inakadiriwa kuwa mnamo karne ya 21, kulikuwa na wachazaji mpira wapatao milioni 250 kati ya watu bilioni 1.3 Duniani. Mwaka 2010 hadhira ya televisheni ya zaidi bilioni 26 ilitazama mashindano ya kwanza ya kombe ya Soka, fainali za Kombe la Dunia za mwezi wa nne.
Licha umaarufu nakupendwa
kwake hakukuwa na timu za wanawake na hii nikutokana na asili ya mchezo huo
kuchezwa na wanaume huku baadhi ya mataifa kutokana na Mila na Tamaduni zao wakiami
wanawake kushiriki katika mchezo huo ni kwenda kinyume na mil ana tamaduni zao.
Lakini mnamo karne ya 19 timu
za mpira wa miguu zikaanzishwa katika mataifa mbali mbali ulimwenguni na
hatimae mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake duniani ukawa ni mchezo rasmi kwao
na kuweza kushiriki michuano mbali mbali ya kikanda, kitaifa na kimataifa.
Na sasa Dunia kushuhidia wachezaji soka bora wakike kama vile Atiana Bonmati, Sam Kerr na Salma Paralluelo wakiwa mabingwa wa kucheza soka Duniani mwaka 2023/2024, ambapo kwa upande wa Barani Afrika kwa mujibu wa jarida la GOAL mchezaji wat imu ya wanawake ya Tanzania Clara Luvaga anaingia kwenye orodha ya wachezaji soka bara 25 Duniani.
Tamasha Ali Omar mwenye umri wa miaka 50, Mkaazi wa Miti Ulaya Wete ni
miongoni mwa wanawake ambao michezo iko ndani ya damu yake, kwani alianza
kushiriki michezo mbali mbali kama vile mpira wa Kikapu, mpira wavu, urushaji
Tufe, riadha nakadhalika tangu akiwa darasa la tatu Skuli ya Miti Ulaya
Kisiwani Unguja akiwa wastani wa umri wa miaka 12 mwaka 1974, na kuendeleza
kukaza msuli hadi akiwa Sekondari Skuli ya Utaani Wete Pemba ambapo alifanikiwa
kushiriki mashindano mbali mbali ya kikanda na kitaifa
Tamasha alisema licha ya
wanawake wengi kukumbana na vihunzi kadhaa wanaposhiriki kwenye michezo hususan
mpira wa miguu lakini kwake imekuwa ni tofauti kwani alipata baraka zote kutoka
kwenye familia yake, walimu wa skuli n ahata jamii iliyokuwa inamzunguka
“Kiupande wangu nashukuru sana kwa kipindi nilipokuwa mdogo sikukumbana na changamoto zozote kwasababu familia yangu ni familia ya michezo kwahivyo sikupata vikwazo kutoka kwa wazazi wangu wala wanajamii na ndio maana nikadumu kwenye michezo kutoka kuwa mchezaji hadi kocha na kuhusu kuwa na tabia mbaya sio kwasababu ya michezo bali khula ya mtu hata asishiriki kwenye michezo” alisema
Kwasasa Tamasha ni mama wa Watoto wanne akiwa na umri wa miaka 50, akiwa kocha wat imu ya mpira wa miguu ya wanawake inayofahamika kwa jina la Wete Women Club, ikiwa na wachezaji 25 na mjumbe wa Soka la Wanawake Zanzibar.
Amesema ukosefu wa Kiwanja rasmi cha kufanyia mazoezi, ukata wa fedha pamoja na maneno yasiyofaa kwa wasichana na wanawake wanaoshiriki mchezo Soka ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Timu ya Wete Women Club, hivyo ameiomba Serikali na wadau wa Soka Visiwani Zanzibar kuboresha mazingira ya Wana michezo wanawake Ili waweze kushiriki katika michezo pasi na vikwazo.
Akizungumzia mafanikio
aliyoyapata kutokana na michezo alisema amefanikiwa kushiriki mashindano mbali
mbali ndani nan je ya Visiwa vya Zanzibar, kujipatia fedha, umaarufu pamoja kuwa
na afya imara mithili ya chuma cha pua.
Aisha Haji Ali na Mafunda Hamad Shehe maarufu Nipe wakaazi wa Miti Ulaya Wete ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya Wete
Women Club, walisema wanamshukuru Bi. Tamasha kuanzisha timu hiyo kwani
inawasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua, kuendeleza na kuwaisaidia wasichana na
wanawake wenye vipaji vya kucheza mpira katika Mkoa wa Kaskazini Pemba hasa Mji
wa Wete
Lakini licha kuanzishwa
kwa timu hiyo walisema wanakumbana vikwazo mbali mbali vikiwemo vya kurudishwa
nyuma ya kushiriki kwenye mchezo huo kwa kisingizio cha kukiuka mila na
utamaduni licha kuvaa mavazi ya stara.
Walisema “kwakweli tunamshukuru sana kocha wetu Bi. Tamasha kwa kuanzisha timu ya mpira ya wanawake kwasababu imeweza kutusaidia sana sisi wanasoka wanawake licha ya kwamba tunakumbana na vikwazo mbali mbali kutoka kwa wanajamii lakini hatujali kwavile tunaona faida ya tunachokifanya”
Mustafa Hassan Suleiman, ni
mume wa Tamasha na Kocha maarufu Visiwani Zanzibar wa Soka Zanzibar alisema tangu afunge ndoa na nguli huyo wa michezo na kocha wat
imu ya mpira ya wanawake hajawahi kuona mabadiliko yoyote ya tabia zisizomridhisha
na kwamba ameridhia kushiriki kwenye michezo kutokana na faida mbali mbali
anazozipata ikiwemo umaarufu, fedha na kuwa afya bora.
“Binafsi tangu nifunge
ndoa na Tamasha sijawahi kuona labda amevaa mavazi yanayokwenda kinyume na
mila, utamaduni na silka zetu Wazanzibari na sio baada ya kufunga nae ndoa hata
kabla ya ndoa kwahivyo nimempa rukhsa na ridhaa kufanya shughuli zake za
michezo nak ama unavyojua kuwa ni kocha wa timu ya mpira wa miguu ya wanawake na
inafanya vizuri katika mashindano mbali mbali lakini pia tangu niishi na
Tamasha sio aghalabu kumsikia anaumwa sijui homa, presha, sukari nakadhalika na
ana miaka 50 sasa” alisema
Mwandishi wa Makala haya,
alifanikiwa kuzungumza na baadhi ya wananchi na majirani wa Tamasha ambapo wote
walithibitisha kuwa kushiriki michezo kwa mama huyo hakujaathiri hata chembe ya
Mila na Utamaduni wa maeneo hayo aidha kutokana na mavazi yake au vitendo
vyengine vya visivyo vya maadili.
Asha Hussein Omar, ni
miongoni mwa majirani wa nguli huyo wa michezo alisema “Mimi tangu kuhamia hapa
namfahamu Tamasha kama mwanamke anayependa michezo sana kila siku saa 12
asubuhi na saa 11 jioni anatoka na vijana wanakwenda mazoezi lakini sijawahi
kumuona amevaa mavazi yasiyo ya staha au kusikia labda ana tabia mbaya za uhasharati
nadhani tabia hizo zinatokana na mtu mwenyewe hata asiwe mwana michezo”
Kuna haja kwa Serikali na wadau wa Michezo Visiwani Zanzibar kufumbua macho upya kuangalia uboreshwaji wa mazingira ya michezo kwa wasichana na wanawake ikiwemo ujengwaji na uboreshwaji wa viwanja, kuandaa makocha, pamoja na kuwepo kwa Sera ya usawa wa Kijinsia kwenye michezo.
Comments
Post a Comment