Vyombo vya habari vina dhima na jukumu la kusaidia katika kuimarisha demokrasia.
Kutoka Dodoma.
Waziri mkuu mstaafu jaji Joseph Warioba.
Vyombo vya habari vina dhima na jukumu la kusaidia katika kuimarisha demokrasia hususan katika kuelimisha umma masuala ya uchaguzi ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika uchaguzi na kuimarisha demokrasia ya ushiriki wa wananchi kwa ukamilifu.
Akizungumza katika kongamano la wadau wa habari na uchaguzi Tanzania lillilofanyika leo katika ukumbi wa hoteli ya Dodoma Waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba alisema kuwa nguvu ya vyombo vya habari havina budi kutumika katika mchakato wa uchaguzi tokea kujiandikisha hadi kupiga kura ili kuimarisha shughuli hizo za uchaguzi.
Jaji warioba alisema kuwa bado vyombo vya habari havikufanya kazi zake kwa ukamilifu katika chaguzi zilizopita hivyo kuna haja ya kubadilika katika vyombo vyetu vya habari ili viweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
“Vyombo vya habari vinatoa habari sio elimu na vinajikita zaidi katika matokeo na havifanyi utafiti”, alifafanua.
Jaji Warioba alisema kuwa enzi zile vyombo vya habari hususan katika maoni ya mhariri vilijikita katika utafiti wa kina na kufanya uchambuzi ambao ulisaidia kuizindua serikali na kuweka sera ambazo zinasaidia kataika kujenga na kuimarisha haki na demokrasia katika masuala mbali mbali.
Alisisitiza haja ya vyama vya siasa kuwa na mawanda mapana katika kuimarisha demokrasia hapa nchini hususan katika hatua za awali za uteuzi wa wagombea.
“Vyama vya siasa viimarishe demokrasia katika uteuzi wa wagombea tuwapelekee wananchi wagombea wanaokubalika kwa wananchi”,
AliongezaAlitoa wito maalum kwa vyombo vya habari kusaidia kupunguza changamoto za uchaguzi katika hatua zote tokea kujiandikisha, kupiga kura pamoja na kuchagua wagombea ambao wamekubalika kwa wananchi.
Vurugu katika uchaguzi zinatokea kutokana na kwamba wananchi hawakuridhika na mchakato wa uchaguzi na sauti na kero zao hawana pahala za kuzitoa hivyo ni muhimu kulitazama kwa kina suala hili la uchaguzi katika hatua zote ili usawa, haki na uwajibikaji uweze kupatikana katika hatua zote.
Katibu Mtendaji wa Baraza la habari Tanzania Ernest Sungura alisema kuwa Baraza la habari Tanzania limejikita katika kukuza maadili na weledi kwa waandishi wa habari ili waweze kutumia kalamu zao katika kujenga misingi ya haki , uwazi na uwajibikaji katika hatua zote za uchaguzi.
Alisema kuwa nguvu ya vyombo vya habari havina budi kutumika kujenga jamii iliyo bora na imara ili lengo la vyombo hivyo katika kuelimisha umma liweze kutekelezwa.“Kuongeza elimu kwa wapiga kura itakayowasaidia kufanya maamuzi makini na sahihi katika sanduku la kupiga kura”, alifafanua.
Alisisitiza kuwa kwa kipindi vyombo vya habari Tanzania havikuwa na mshikamano na maandalizi ya pamoja na kuimarisha habari za uchaguzi katika hatua zote ili kuimarisha elimu kwa wapiga kura lakini pia wananchi waweze kupata taarifa ambazo zitawasaidia katika kufanya uamuzi wakati wa kupiga kura.
“Vyombo vya Habari vya Tanzania huwa havina maandalizi ya Pamoja ya namna ya kuandika na kutangaza Habari za uchaguzi katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kuanzia uboreshaji wa daftari la wapiga kura, kujiandikisha kwa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, elimu kwa mpiga kura, kampeni hadi siku ya kupiga kura”.
AlifafanuaHivyo alisema kuwa Baraza la habari linakusudia Kuviandaa vyombo vya Habari mapema kwa kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa unaolenga kuvisaidia vyombo vya Habari kufanya kazi ya kihabari ya kutoa taarifa sahihi kwa wakati sahihi kufichua uovu na kuwajibisha na kuibua masuala ili yajadiliwe.
Mwakilishi wa ubalozi wa Marekani Kalisha Holmes, alisema kuwa vyombo vya habari ni muhimili wa nne na hivyo vina wajibu wa kuelimisha umma katika masuala ya uchaguzi ili waweze kufanya maamuzi sahihi.Katika kipindi hiki ni wakati muafaka wananchi kupata habari zilizo sahihi ili waweze kufuatilia kwa karibu hatua zote za kuimarisha demokrasia pamoja na kutumia vyombo vya habari kama njia muhimu ya kuimarisha demokrasia hususan katika kuelekea uchaguzi.
“Umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari unahitajika. Vyombo huru na vinavyojitegemea ni nguzo muhimu katika kukuza na kuimarisha demokrasia”, aliongeza.
Wakichangia katika kongamano hilo Usia Nkhoma Mtaalam wa mawasiliano kutoka UNICEF alisema kuwa Vyombo vya habari viwe na agenda ili viakisi maoni na matakwa ya wananchi ili tuwe na vyombo vya habari makini, tunalo jukumu kubwa la namna gani tunaweza kujenga vyombo vya habari imara ambao tulazimishe wanasiasa waweke masuala ambayo yanayokidhi mahitaji ya vizazi vyetu.
Edda Sanga mwandishi mkongwe alisema wanawake hawana budi kupewa fursa ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa matakwa yao na kamwe wasitumike kama ngazi katika uchaguzi.
Sauti za walioko pembezoni pia ziweze kupewa nafasi katika uchaguzi na kero zao ziibuliwe na kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.Pili Mtambilike mtaalamu wa sekta ya habari amesema vyombo vya habari vina dhima kubwa ya kuondoa sumu iliyojengeka katika uchaguzi na hivyo kuongeza elimu ya wapiga kura katika vyombo vya habari. Vyombo vya habari viwe mstari wa mbele katika kusaidia kueneza suala hilo la elimu kwa mpiga kura.
Aliongeza umuhimu wa makundi yote ya pembezoni kuwemo katika hatua zote za uchaguzi hususan makundi ya walemavu ili kuimarisha ushiriki wa watu wote katika masuala ya uchaguzi. Mchakato wa kuwapata wagombea katika makundi hayo uwe wa uwazi na uzingatie haki na usawa kwa wote. Kongamano hilo la siku moja ambalo limefanyika leo katika ukumbi wa Dodoma Hotel likiwa na kauli mbiu ya uandishi wa habari za uchaguzi kwa weledi na kujenga usawa, haki na uwajibikaji limeandaliwa na Baraza la habari Tanzania na limewashirikisha wadau wa habari, wanasiasa, waandishi wa habari pamoja na asasi za kiraia.
Hii ni mara ya kwanza kwa kongamano la aina hiyo kufanyika hapa nchini likiwa na lengo la Kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja kuongeza UWAZI, HAKI na UWAJIBIKAJI tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025. Kongamano hilo limefadhiliwa na Ubalozi wa Marekani na IFES (The international and Foundation for Electoral system).
Comments
Post a Comment